Kiongozi wa Hizbullah: Muqawama hautasalimu amri wala kurudi nyuma katika kulinda mamlaka ya Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i140684-kiongozi_wa_hizbullah_muqawama_hautasalimu_amri_wala_kurudi_nyuma_katika_kulinda_mamlaka_ya_lebanon
Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbollah amesema kuwa, Muqawama hautakubali kusalimu amri wala kurudi nyuma katika kulinda mamlaka, heshima na umoja wa ardhi ya Lebanon, akiongeza kuwa Israel na Marekani zimekuwa zikiilazimisha Beirut kutekeleza matakwa yao na kudhoofisha mamlaka ya nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2026-08-15T10:57:40+00:00 )
Aug 15, 2026 10:56 UTC
  • Kiongozi wa Hizbullah: Muqawama hautasalimu amri wala kurudi nyuma katika kulinda mamlaka ya Lebanon
    Kiongozi wa Hizbullah: Muqawama hautasalimu amri wala kurudi nyuma katika kulinda mamlaka ya Lebanon

Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbollah amesema kuwa, Muqawama hautakubali kusalimu amri wala kurudi nyuma katika kulinda mamlaka, heshima na umoja wa ardhi ya Lebanon, akiongeza kuwa Israel na Marekani zimekuwa zikiilazimisha Beirut kutekeleza matakwa yao na kudhoofisha mamlaka ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Sheikh Naim Qassem amesema kuwa masharti ya utawala haramu wa Israel ya kuidhinisha kupelekwa jeshi la Lebanon, ikiwemo kulifanya jambo hilo kutegemea matokeo ya kamati za uchunguzi, ni tusi dhidi ya mamlaka ya kitaifa ya Lebanon.

Katibu Mkuu wa Hizbullah pia ameikosoa serikali ya Lebanon kwa msimamo wake wa kuafikiana na kauli za maafisa wa Israel, akiwemo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wa Vita Israel Katz, na kuitaka Beirut itathmini upya msimamo wake.

Sheikh Qassem amesema kuwa, kukubali Lebanon kile kinachoitwa “makubaliano ya fremu” chini ya shinikizo la Marekani hakukuwa makubaliano yenye usawa, bali kulikuwa kusalimu amri mbele ya matakwa ya Israel na kurudi nyuma katika kulinda mamlaka ya kitaifa. Amesema makubaliano hayo hayakuleta manufaa yoyote kwa maslahi ya kitaifa ya Lebanon na kwamba Hizbollah ilikataa makubaliano hayo.

Kiongozi huyo alikataa pia kuielezea Marekani kama mpatanishi, akisema kuwa Washington na Israel zinafanya kazi upande mmoja.

Sheikh Qassem pia amesema kuwa Hizbollah ilifanya operesheni ya makombora kujibu kuuawa shahidi Kiongozi wa zamani wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatollah Sayyid Ali Khamenei, pamoja na ukiukaji wa makubaliano uliofanywa na Israel kwa muda wa miezi 15 mfululizo.

Kiongozi huyo mwandamizi wa Hizbullah ameeleza pia kuwa uchokozi wa Israel dhidi ya Lebanon ulikuwa umepangwa mapema na ungeendelea kutekelezwa hata kama Muqawama usingetoa majibu.