Kiongozi wa muqawama ataka kuhitimishwa udhibiti wa moja kwa moja wa kifedha wa Marekani kwa Iraq
-
Abu Ala al- Walai; Katibu Mkuu wa Kata’ib Sayyid al-Shuhada
Katibu Mkuu wa kundi la muqawama la Iraq la Kata’ib Sayyid al-Shuhada amekosoa vikali udhibiti wa moja kwa moja wa Marekani wa fedha na uchumi na mali za Iraq na kutaka kutafutwa masoko mbalimbali ya mauzo ya nje, kuimarisha uhusiano wa kibenki na kuhitimisha kivitendo udhibiti wa kifedha wa Washington kwa nchi hiyo ya Kiarabu.
"Miongoni mwa vipengele vinavyoonekana wazi zaidi vya kupotea kwa mamlaka kamili ya utawala wa serikali ya Iraq ni namna Marekani inavyodhibi uchumi na kuwa na sauti kwa mapato na mali za nchi, unyakuzi wake kamili wa rasilimali za Iraq na kuikalia kwa mabavu nchi yetu," ameeleza Abu Ala al-Walai katika chapisho alilotuma katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X, Jumamosi usiku.
Ameongeza kuwa "taifa tukufu la Iraq" halitakubali rasilimali zake za asili kuporwa na kutotambuliwa kama haki halali ya kitaifa.
Katibu Mkuu wa Kata’ib Sayyid al-Shuhada ameeleza kuwa mamlaka kamili ya kujitawala haipatikani tu kwa kudhibiti ardhi, bali inahitaji pia uwezo wa kufanya maamuzi katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kifedha bila ya udhibiti wa nguvu yoyote ya dola ajinabi.
Tangu ilipoivamia Iraq mwaka 2003, Marekani imekuwa ikidhibiti sehemu kubwa ya mapato ya mafuta ya nchi hiyo huku ikiwa na mamlaka makuu kwa masuala mbalimbali ya serikali ya Baghdad.
Marekani inadhibiti mapato ya mafuta ya Iraq kutokana na kusimamia pakubwa mapato hayo kupitia Benki ya Hifadhi ya Shirikisho ya New York.
Chanzo kikuu cha mapato ya Iraq ni mafuta, ambayo yanachangia asilimia 90 ya bajeti ya nchi hiyo.