Kuanzia Uhamiaji hadi Kukimbia: Jinsi Ndoto ya Kizayuni ya "Nchi ya Ahadi" Ilivyoporomoka
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i140724-kuanzia_uhamiaji_hadi_kukimbia_jinsi_ndoto_ya_kizayuni_ya_nchi_ya_ahadi_ilivyoporomoka
Hali ya walowezi wa Kizayunu kukimbia ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, zinazodaiwa kuwa Israel, na kurejea katika nchi walikotoka imekuwa ishara ya wazi ya mmomonyoko wa ndani wa mradi wa Kizayuni.
(last modified 2026-08-17T05:27:50+00:00 )
Aug 17, 2026 05:25 UTC
  • Kuanzia Uhamiaji hadi Kukimbia: Jinsi Ndoto ya Kizayuni ya

Hali ya walowezi wa Kizayunu kukimbia ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, zinazodaiwa kuwa Israel, na kurejea katika nchi walikotoka imekuwa ishara ya wazi ya mmomonyoko wa ndani wa mradi wa Kizayuni.

Watu waliohamia Palestina kutoka sehemu mbalimbali za dunia kwa miongo kadhaa ili kuweka misingi ya utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina, sasa wanakimbia na kuondoka katika ardhi hizo. Suala hapa si idadi tu ya wahamiaji wanaoondoka; umuhimu halisi upo katika ni nani anayeondoka na kwa nini hawaoni tena mustakabali wao na wa watoto wao ukiwa katika ardhi hizo zilizoghusubiwa.

Ripoti za vyombo vya habari vinavyoaminika zinaonyesha kuwa takriban watu 150,000 wamekimbia na kuondoka katika ardhi hizo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, hali iliyopelekea uwiano wa uhamiaji wa utawala wa Kizayuni kuwa hasi katika miaka ya 2023 na 2024. Sergio DellaPergola, mtaalamu mashuhuri wa masuala ya idadi ya watu, ameelezea hali hii kama jambo la kipekee katika historia ya idadi ya watu ya utawala wa Kizayuni.

Umuhimu wa jambo hili unadhihirika zaidi ikizingatiwa kuwa uhamiaji wa Wayahudi kutoka sehemu mbalimbali duniani umekuwa kichocheo kikuu cha ongezeko la idadi ya Wazayuni huko Palestina. Kati ya mwaka 1948 na 1960, uhamiaji ulichangia takriban asilimia 65 ya ongezeko la idadi ya watu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu; hata hivyo, leo hii hali hiyo imebadilika na kuwa kinyume kabisa. Hali hii haiwezi kuhusishwa na vita vya Gaza na ukatili mkubwa uliofanywa dhidi ya Wapalestina pekee. Mgogoro wa kisiasa uliotokana na mpango wa baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu wa kufanyia marekebisho mfumo wa mahakama ulikuwa tayari umejitokeza kabla ya kuanza vita hivyo. Baadaye, vita vya Gaza, pamoja na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama, uhamasishaji mkubwa wa askari wa akiba, mashinikizo ya kiuchumi na kuongezeka kwa migawanyiko ya kijamii, vilichochea kasi ya watu kuondoka.

Kwa hivyo, vita hivyo haviwezi kuchukuliwa kuwa chanzo kikuu cha migogoro yote inayoukabili utawala wa Kizayuni bali, vimefichua na kuzidisha tu migogoro na migawanyiko ya ndani ambayo utawala huo tayari ulikuwa unakabiliwa nayo.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Tel Aviv unaonyesha kuwa zaidi ya watu 100,000 waliokimbia ardhi zinazokaliwa kwa mabavu katika miaka ya 2023 na 2024, na idadi ya wanaoondoka sasa imefikia makumi ya maelfu ya watu.

Hata hivyo, umuhimu mkubwa wa takwimu hizi haupo tu katika idadi ya watu wanaokimbia, bali katika muundo wa watu wanaohama. Wataalamu wa teknolojia, madaktari, wahandisi, wasomi, wawekezaji na wataalamu wenye elimu ya juu wanaunda sehemu kubwa ya wale wanaoondoka.

Mgogoro wa uhamiaji sasa umebadilika kutoka kuwa suala la idadi ya watu na kuwa changamoto ya kimkakati. Utawala wa Kizayuni unapoteza si idadi ya watu pekee, bali pia mtaji wake wa rasilimali watu. Uchumi wake unategemea sana teknolojia za kisasa na nguvukazi yenye ujuzi. Hivyo, kuhama kwa madaktari, wahandisi na wataalamu wa sayansi na teknolojia kunatishia kupunguza uwezo wa uzalishaji, ubunifu na mapato ya kodi. Uchunguzi uliofanywa na taasisi za Israel pia umeonya kuhusu kuongezeka kwa uhamaji wa watu matajiri na wataalamu. Kuendelea kwa mwelekeo huu kunaweza kupunguza mapato ya kodi na kuweka mzigo zaidi kwenye uchumi na bajeti ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni inayokumbwa na matatizo ya vita.

Taasisi ya Masomo ya Usalama wa Taifa (INSS) na Taasisi ya Demokrasia ya Israel pia zimeonya kuhusu matokeo hasi ya kuhama wataalamu na mwelekeo unaoongezeka wa kuhama vijana na watu wenye kipato cha juu.

 

Jambo jingine muhimu ni kupungua kwa viwango vya ubora wa maisha. Gharama kubwa za kodi za nyumba, mashinikizo ya kiuchumi, ukosefu wa usalama, na kutokuwa na utulivu wa kisiasa kumefanya maisha nje ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kuwa ya kuvutia zaidi kwa sehemu kubwa ya Wazayuni. Pamoja na hayo, kuna mgogoro mkubwa zaidi katika kiini cha mambo hayo yote ambao unahusu mustakabali wa mradi wa Kizayuni. Hofu kuhusu mustakabali wa kisiasa, kuongezeka makundi yenye misimamo mikali, migawanyiko inayozidi kuongezeka katika jamii, na zaidi ya yote, mustakabali wa watoto wao, vimefanya baadhi ya walowezi kuamua kuhama.

Kwa mradi wa Kizayuni, hali hii ni kitendawili cha kihistoria. Utawala ulioanzishwa kwa kuhamisha na kuwawapa makazi walowezi wa Kiyahudi kutoka sehemu mbalimbali za dunia katika ardhi zilizoporwa za Palestina, sasa unakabiliwa na hali ya sehemu kubwa ya walowezi hao hao kukimbia ardhi hizo. Gilad Kariv, mbunge wa Knesset na mwenyekiti wa Kamati ya Uhamiaji na Ujumuishaji, ameelezea hali hii ya sasa kama "tsunami" na tishio kwa uthabiti wa utawala huo.