Ansarullah: Uhalifu wa Israel nchini Lebanon na Palestina unafanywa kwa idhini ya Marekani
Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah nchini Yemen imelaani mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya maeneo ya kusini mwa Lebanon.
Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah pia imelaani mashambulizi yanayoendelea ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, ikisisitiza kuwa kuwalenga raia nchini Lebanon, Gaza na Ukingo wa Magharibi, pamoja na kuendelea ongezeko la mivutano linalofanywa na utawala wa Israel na viongozi wake, ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu.
Ansarullah imesema vitendo hivyo vya Israel vinafanyika kwa “msaada na himizo la wazi kutoka Marekani”, huku vikitekelezwa chini ya ushirikiano na ukimya wa baadhi ya serikali za Kiarabu ilizozitaja kuwa vibaraka.
Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah imesisitiza mshikamano wake na wananchi wa Palestina na Lebanon, pamoja na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah, ikisema Lebanon na muqawama wake vina “haki ya kujibu uchokozi wa Israel na kuwalinda wananchi wa Lebanon.
Harakati hiyo pia imeeleza masikitiko yake kuhusu kuendelea mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Serikali ya Lebanon na utawala wa Kizayuni, ikisema mazungumzo hayo yanaweza kusababisha Lebanon kutoa masharti na makubaliano kwa gharama ya maslahi na heshima ya wananchi wake.
Ansarullah imeitaka Serikali ya Lebanon kutathmini upya msimamo wake na kutumia nguvu ya muqawama wa Kiislamu kama nyenzo ya kulinda nchi.
Ofisi hiyo pia, ikizungumzia utendaji wa muqawama wa Kiislamu nchini Lebanon, imesisitiza kuwa muqawama huo umeweka “rekodi nzuri ya ushindi wa kihistoria” katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni.