Vitisho Visivyo na Uzito vya Trump na Kudhoofika kwa Nguvu ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i140896-vitisho_visivyo_na_uzito_vya_trump_na_kudhoofika_kwa_nguvu_ya_marekani
Rais Donald Trump wa Marekani kwa mara nyingine tena ametishia kuishambulia Oman kwa mabomu, nchi iliyo na nafasi muhimu katika mazungumzo yanayohusu Iran pamoja na masuala yanayohusiana na usafiri wa baharini katika Lango Bahari la Hormuz.
(last modified 2026-08-23T05:02:58+00:00 )
Aug 23, 2026 04:57 UTC
  • Vitisho Visivyo na Uzito vya Trump na Kudhoofika kwa Nguvu ya Marekani

Rais Donald Trump wa Marekani kwa mara nyingine tena ametishia kuishambulia Oman kwa mabomu, nchi iliyo na nafasi muhimu katika mazungumzo yanayohusu Iran pamoja na masuala yanayohusiana na usafiri wa baharini katika Lango Bahari la Hormuz.

Trump amesema iwapo Oman itazuia hatua za Marekani kuhusu lango hilo, ataishambulia kwa mabomu mazito. Tishio hili haliwezi kupuuzwa kama kauli ya kawaida tu katika sera ya mambo ya nje ya Marekani, bali ni sehemu ya mwenendo ambao umeshuhudia ongezeko la vitisho vyenye maneno makali visivyotekelezwa kivitendo. Hivyo, halitakuwa jambo la kushangaza iwapo Oman haitachukulia kwa uzito vitisho hivyo vya Trump. Historia ya utawala wa Trump katika mahusiano yake na mataifa mbalimbali inaonyesha kuwepo kwa tofauti kubwa kati ya vitisho na hatua halisi zinazochukuliwa. Pengo hili sasa limegeuka kuwa tatizo la kimkakati kwa Washington.

Trump anajaribu kugeuza "kutotabirika" kwake kuwa wenzo wa kuimarisha nguvu ya Marekani. Hata hivyo, bila ya uwepo wa mkakati madhubuti, hali ya kutotabirika hubadilika taratibu kuwa "kutokuaminika." Washirika huachwa gizani kuhusu hatua inayofuata ya Washington, huku wapinzani wakizidi kutambua ni vitisho vipi vinavyoweza kutekelezwa na vipi vinakusudiwa tu kutoa mashinikizo ya kisiasa dhidi ya mahasimu wake.

CNN inaona kuwa wigo wa mgogoro huu unavuka mipaka ya Iran ambapo sasa Oman inakabiliwa na tishio la kijeshi, huku Korea Kusini ikiendelea kuwa chini ya mashinikizo ya Washington. Trump anaikosoa Seoul kwa kukataa kujiunga na vita dhidi ya Iran na wakati huo huo kuchukua misimamo hasi kuhusu mazoezi ya kijeshi ya Marekani na Korea Kusini ambayo inaendana na baadhi ya matakwa ya Korea Kaskazini. Mkanganyiko huu unaweza kutuma ishara hatari kwa washirika wa Marekani kwamba Washington inatarajia ushirikiano kutoka kwao lakini inatuma ujumbe kinzani kuhusu ahadi zake za kiusalama.

Kuhusiana na suala hili, Trump anaichukulia zaidi miungano kama mikataba ya kifedha kuliko ilivyokuwa huko nyuma, ambapo sasa mshirika anatarajiwa kulipa gharama na kushirikiana kikamilifu na Washington katika operesheni zake zote za kijeshi. Mtazamo huu unabadilisha muungano kutoka kuwa uwekezaji wa kimkakati wa muda mrefu hadi muamala wa kibiashara tu wa muda mfupi.

Richard Haass, mkuu wa zamani wa Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Marekani, pia ameonya dhidi ya mwelekeo huu. Ameelezea madai ya Trump kuhusu umiliki wa Marekani wa Lango Bahari la Hormuz kuwa ya "kipuuzi" na "yenye madhara." Marekani imekuwa ikisisitiza kwa muda mrefu hadhi ya kimataifa ya njia hiyo ya maji, na madai ya namna hiyo yanapingana wazi na msimamo wa muda mrefu wa sera za kigeni za Washington.

Haass pia anaona hatua ya kuhamishwa rasilimali za kijeshi za Marekani kutoka Asia Mashariki hadi Asia Magharibi kuwa jambo hatari. Kwa mtazamo wake, hatua hiyo inaweza kuzidisha wasiwasi miongoni mwa Japan, Korea Kusini, Australia, na Ufilipino, huku wakati huo huo ikitoa fursa zaidi kwa China na Korea Kaskazini kupanua ushawishi wao katika eneo hilo.

Wasiwasi huu si wa kinadharia tu. Korea Kaskazini inaendelea kuimarisha mipango yake ya nyuklia na makombora, ambapo uhusiano wa Pyongyang na Moscow pamoja na Beijing umeimarika zaidi. Russia imetupilia mbali mipango ya Trump ya kuhitimisha vita na Ukraine, nayo China haijalegeza msimamo katika ushindani wake wa kiuchumi na kimkakati na Marekani.

Hivyo basi, tatizo la sera za mambo ya nje za Trump si wingi wa vitisho pekee bali suala la msingi ni kukosekana mkakati madhubuti unaoziongoza sera hizo. Trump anajaribu kufikia malengo na matakwa yake kutoka upande wa pili kupitia mashinikizo, huku akighafilika na ukweli kwamba mashinikizo makubwa kupita kiasi kwa washirika yanaweza kuwasukuma mbali na Marekani. Aidha, vitisho vya mara kwa mara dhidi ya wapinzani hupoteza uwezo wake wa kiutendaji pale vinapotolewa mara kwa mara bila kufuatiwa na utekelezaji wa kivitendo.

Si kwamba Marekani kwa sasa haina nyenzo za nguvu na ushawishi, tatizo kuu ni kudhoofika na kutoweka kwa imani na uhalali unaoambatana na matumizi ya nguvu hizo. Mshirika anayepoteza imani na ahadi za Marekani atatafuta njia mbadala, huku mpinzani wake akiona fursa katika kusita kwa Washington na hivyo kujiamini zaidi.

Kuanzia Oman hadi Korea Kusini, hali inayojitokeza ni moja: Trump anataka dunia iogope nguvu ya Marekani, lakini ni wazi kuwa sera inayotumia vitisho badala ya mkakati madhubuti inaweza kuleta matokeo kinyume na inavyotarajiwa.

Dunia ikihitimisha kuwa Washington hutoa vitisho zaidi kuliko kuchukua hatua, gharama ya hali hii kwa Marekani inaweza kuwa kubwa zaidi hata kuliko ya operesheni ya kijeshi iliyoshindwa. Katika siasa za kimataifa, kuporomoka halisi kwa nguvu huanzia pale wengine wanapoacha kuchukulia kwa uzito vitisho vya taifa lenye nguvu.