Mwisho wa satwa ya Marekani: Asia Magharibi Katika Ukingo wa Mfumo Mpya
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i140898-mwisho_wa_satwa_ya_marekani_asia_magharibi_katika_ukingo_wa_mfumo_mpya
Katika uchambuzi wake wa hivi karibuni, jarida la Foreign Affairs linataja vita dhidi ya Iran kama hatua muhimu inayoharakisha kuporomoka kwa mfumo wa kikanda unaoongozwa na Marekani na kudhihiri taratibu mabadiliko yanayoweza kubadili mitazamo na mikakati ya kiusalama ya mataifa ya Asia Magharibi katika miaka ijayo.
(last modified 2026-08-23T16:27:57+00:00 )
Aug 23, 2026 06:27 UTC
  • Mwisho wa satwa ya Marekani: Asia Magharibi Katika Ukingo wa Mfumo Mpya

Katika uchambuzi wake wa hivi karibuni, jarida la Foreign Affairs linataja vita dhidi ya Iran kama hatua muhimu inayoharakisha kuporomoka kwa mfumo wa kikanda unaoongozwa na Marekani na kudhihiri taratibu mabadiliko yanayoweza kubadili mitazamo na mikakati ya kiusalama ya mataifa ya Asia Magharibi katika miaka ijayo.

Tathmini hii inavuka mipaka ya matokeo ya mgogoro wenyewe. Inaashiria kuporomoka taratibu mfumo ambao Washington iliujenga kwa miongo kadhaa kwa madai ya kudhamini usalama katika eneo la Asia Magharibi, mfumo uliotegemea uwepo mkubwa wa kijeshi wa Marekani, uanzishwaji wa kambi nyingi, ahadi za usalama kwa washirika wake wa Kiarabu, uungaji mkono kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na jitihada za kuizuia Iran kujiimarisha.

Mambo haya yenyewe sasa yamekuwa sababu zinazodhoofisha hadhi ya Marekani kuliko wakati mwingine wowote. Vita dhidi ya Iran vimefichua ukweli muhimu kwa mataifa ya Kiarabu nao ni kwamba kuwepo vikosi na kambi za kijeshi za Marekani katika eneo la Magharibi mwa Asia hakuyadhaminii usalama unaohitajika.

Wakati wa mzozo huu, nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi zimekabiliwa na madhara ya moja ya vita hivyo, ingawa uamuzi wa kuanzisha vita vyenyewe ulifanywa na Washington na Tel Aviv. Kwa hakika, Marekani ilianzisha vita katika Ghuba ya Uajemi lakini ikashindwa kuyakinga mataifa ya kusini mwa ghuba hiyo na madhara yake. Umuhimu wa jambo hili unadhihirika zaidi pale tunapozingatia suala la Lango-Bahari la Hormuz. Kwa miongo kadhaa, sababu kuu ya uwepo wa jeshi la Marekani Asia Magharibi imedaiwa kuwa ni kuhakikisha mtiririko huru wa nishati na kulinda njia muhimu za biashara. Hata hivyo, vita hivi vimeonyesha kuwa Washington inakabiliwa na changamoto kubwa katika kushughulikia vurugu au vikwazo vinavyoathiri njia hii muhimu ya majini.

Katika tathmini za hivi karibuni, jarida la Foreign Affairs linaeleza kuwa kufungwa Lango-Bahari la Hormuz ni mbinu iliyotumiwa na Iran kuhamishia sehemu ya gharama za kiuchumi za vita hivyo kwa mahasimu na washambuliaji wake.

Hali hii inatoa onyo la kimkakati kwa mataifa ya Kiarabu. Kwa sasa yanakabiliwa na hali tata. Ingawa Marekani inadumisha nguvu kubwa ya kijeshi katika kanda ya Asia magharibi, lakini uwepo huo wa kijeshi unaweza kuyafanya kuwa shabaha ya mashambulizi zaidi iwapo mzozo utaongezeka.

Wakati huo huo, matukio yanayoendelea Gaza yamekuwa na mchango mkubwa katika kubadili mitazamo na mahesabu ya nchi za eneo la Asia Magharibi. Uungaji mkono wa wazi wazi wa Washington kwa sera za kikatili za utawala wa Kizayuni wakati wa vita vya Gaza umepanua zaidi pengo lililopo kati ya Marekani na maoni ya umma katika eneo hilo, huku pia ukiibua shaka miongoni mwa serikali kuhusu gharama za kuunga mkono kikamilifu sera za Washington.

Ukosoaji dhidi ya msimamo huu umeongezeka hata ndani ya duru za sera za kigeni za Marekani. Jarida la Foreign Affairs awali lilionya kuwa uungaji mkono usio na masharti wa Washington kwa sera za utawala wa Kizayuni katika vita vya Gaza umedhoofisha uwezo wa Marekani wa kushawishi matukio katika eneo. Kwa hivyo, mataifa ya Asia Magharibi yanasonga mbele, kuliko siku za nyuma, kuelekea kubadilisha uhusiano wao wa kigeni, kupunguza utegemezi wao wa usalama kwa nguvu moja ya kigeni, na kuanzisha mifumo ya kiusalama ya kikanda. Juhudi za karibuni za baadhi ya nchi za kanda za kuunda mipango huru ya usalama ni miongoni mwa ishara za mabadiliko haya.

Bila shaka, mgogoro wa uaminifu kwa Marekani haumaanishi ulazima wa kuibuka nguvu nyingine mbadala ya kimabavu. China na Russia, kwa mfano, zina mapungufu na mambo yao maalumu yanayozishughulisha kwa ndani. Hata hivyo, kwa mara ya kwanza katika miongo kadhaa iliyopita, nchi za eneo hili zinazidi kufikia hitimisho kwamba haziwezi tena kukabidhi usalama wao wote kwa nguvu moja ya kigeni. Washington inaweza kuendelea kudumisha kambi za kijeshi, meli na ndege za kivita, pamoja na maelfu ya askari katika kanda ya Asia Magharibi, lakini ni wazi kuwa nguvu ya kijeshi pekee haiwezi tena kuwa na itibari na ushawishi uleule wa kisiasa iliyokuwa nao huko nyuma.

Vita dhidi ya Iran pia vimefichua ukweli kwamba, ingawa Marekani inaweza kuanzisha vita, lakini haina uwezo wa kudhibiti jinsi vita hivyo vitakavyomalizika au ukubwa wa gharama vitakazowabebesha washirika wake.