Amani ya Kudumu Katika Eneo Itapatikana tu Pale Utawala wa Kizayuni Utakapopokonywa Silaha za Nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141002-amani_ya_kudumu_katika_eneo_itapatikana_tu_pale_utawala_wa_kizayuni_utakapopokonywa_silaha_za_nyuklia
Madamu silaha za nyuklia za utawala wa Kizayuni wa Israel, ambao ndio utawala pekee unaomiliki silaha za nyuklia katika Asia Magharibi, zitaendelea kufunikwa na utata wa makusudi wa utawala huo pamoja na kimya cha kimataifa, mjadala wowote kuhusu upokonyaji silaha katika eneo hautakuwa na maana na utaendelea kuwa ni unafiki mtupu.
(last modified 2026-08-27T06:18:22+00:00 )
Aug 27, 2026 06:12 UTC
  • Amani ya Kudumu Katika Eneo Itapatikana tu Pale Utawala wa Kizayuni Utakapopokonywa Silaha za Nyuklia

Madamu silaha za nyuklia za utawala wa Kizayuni wa Israel, ambao ndio utawala pekee unaomiliki silaha za nyuklia katika Asia Magharibi, zitaendelea kufunikwa na utata wa makusudi wa utawala huo pamoja na kimya cha kimataifa, mjadala wowote kuhusu upokonyaji silaha katika eneo hautakuwa na maana na utaendelea kuwa ni unafiki mtupu.

Ingawa utawala wa Kizayuni haujawahi kuthibitisha au kukanusha rasmi kuwa na silaha za nyuklia, lakini ripoti za kuaminika kimataifa zinaonyesha kwamba utawala huo ghasibu una hazina kubwa ya silaha za nyuklia. Ripoti ya 2025 ya Taasisi ya Utafiti wa Amani ya Kimataifa ya Stockholm (SIPRI) inasema kwamba utawala wa Kizayuni una takriban vichwa 90 vya nyuklia. Akiba hii ya silaha, yenye nguvu ya mlipuko inayofikia mara 165 ya ile ya mabomu yaliyodondoshwa na Marekani huko Hiroshima na Nagasaki, inaleta tishio kubwa kwa usalama wa eneo. Mbali na hayo, utawala huo una uwezo wa kutengeneza takriban vichwa vipya kumi vya silaha hizo kila mwaka. Urundikaji huo wa silaha hatari za maangamizi ya umati katika eneo unalenga kudumisha ubabe wa kijeshi wa Israel na kutishia usalama wa nchi jirani. Kwa upande mwingine, Iran ambayo imekuwa mwanachama wa mkataba wa kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia tangu 1970 na imeweka wazi vituo vyake vya nyuklia kwa ajili ya usimamizi na ukaguzi wa mara kwa mara wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA, inakabiliwa na mashinikizo makubwa ya kisiasa na vikwazo vya kiuchumi kutokana na ubaguzi wa madola makubwa duniani na vilevile kushindwa taasisi za kimataifa kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu na usawa. Licha ya kuwa Azimio nambari 487 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linautaka utawala wa Kizayuni uweke vituo vyake vyote vya nyuklia chini ya usimamizi wa wakala wa IAEA, lakini umekataa na kupuuzilia mbali azimio hilo kwa miaka mingi kutokana na uungaji mkono usio na masharti wa Marekani. Kwa zaidi ya nusu karne sasa, Israel imekuwa ikitumia kila mbinu kwa ajili ya kuhifadhi ukiritimba wake wa nyuklia katika Asia Magharibi, suala ambalo bila shaka linachochea mashindano ya silaha katika eneo.

Utawala wa Kizayuni umekataa kutia saini mkataba wa kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia na hivyo kupinga usimamizi wa kimataifa juu ya vituo vyake vya nyuklia. Theodore Postol, ambaye ni mshauri wa zamani katika Wizara ya Ulinzi ya Marekani, anasema waziwazi kuwa tishio kuu la nyuklia katika eneo la Asia Magharibi halitokani na Iran, bali na Israel. Anasisitiza kuwa, madamu utawala wa Kizayuni utaendelea kukataa kujiunga na Mkataba wa Kutokueneza Silaha za Nyuklia (NPT) na kukubali ukaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), jitihada zozote za kuanzisha eneo lisilo na silaha za nyuklia katika Asia Magharibi zitakabiliwa na kikwazo kikubwa.

Moja ya changamoto za kimsingi katika suala la upunguzaji silaha za nyuklia katika eneo ni siasa za undumakuwili zinazotekelezwa na Marekani kuhusiana na mipango ya nyuklia ya nchi mbalimbali. Washington imetumia rasilimali na nguvu zake zote kulenga mpango wa nyuklia wa Iran kupitia vikwazo vya kiuchumi, mzingiro wa majini na mashambulizi ya kijeshi. Kinyume chake, si tu imezuia kuwekewa mashinikizo utawala wa Kizayuni kuhusu mpango wake wa nyuklia bali pia inaunga mkono siasa za utawala huo za kutoweka wazi mpango huo. Msimamo huu umedhoofisha sana itibari na uwajibikaji wa Marekani kuhusiana na suala zima la kuzuia kuenea duniani silaha za nyuklia. Hata ndani ya Marekani kwenyewe, wabunge kadhaa wameishutumu serikali kwa kuendeleza siasa hizo za kibaguzi na kutaka kuwepo uwazi kuhusu maghala ya silaha za nyuklia za utawala wa Kizayuni. Ikiwa Marekani inasisitiza kuwa Iran haipaswi kumiliki silaha za nyuklia, sharti hilo hilo pia linapaswa kutumika kwa utawala wa Kizayuni.

Jumuiya za kimataifa, zikiwemo Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Umoja wa Mataifa, zimesisitiza mara kwa mara umuhimu wa kuwekwa vituo vya nyuklia vya utawala wa Kizayuni chini ya usimamizi kamili wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Katika azimio lililoungwa mkono na nchi 152, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pia limetoa wito kwa utawala wa Kizayuni kutokomeza silaha zake za nyuklia na kukubali ukaguzi wa IAEA. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na baadhi ya nchi za Kiarabu kama vile Misri, Kuwait na Qatar zimetaka utawala wa Kizayuni ulazimishwe kujiunga na Mkataba wa Kutokueneza Silaha za Nyuklia (NPT) na kukubali usimamizi wa IAEA. Hatua hii inachukuliwa kuwa muhimu sana katika kujenga imani na kupunguza mivutano katika eneo. Kwa ujumla ni kuwa, ikiwa amani ya kudumu itaanzishwa Asia Magharibi, silaha za nyuklia za utawala wa Kizayuni haziwezi kufumbiwa macho. Kutokomezwa kwa silaha za nyuklia za utawala huu na kuwekwa mpango wake wa nyuklia chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) si tu ni hitajio la kisiasa, bali ni sharti la kisheria, kiusalama na kimaadili. Madamu undumakuwili utaendelea kutekelezwa kuhusu silaha za nyuklia na Israel, eneo hili bila shaka litaendelea kubaki limenasa katika mzunguko wa kutokuwa na utulivu na ukosefu wa usalama. Badala ya kukaa kimya, jamii ya kimataifa inawajibika kuushinikiza utawala wa Kizayuni uheshimu sheria za kimataifa na kuchukua hatua za kivitendo katika kutokomeza silaha zake za nyuklia. Ni kwa njia hii tu ndio tunaweza kutumainia kuwa na eneo lisilo na silaha za nyuklia na lililo na amani na utulivu wa kudumu katika Asia Magharibi.