Maulama wa Pakistan: Umoja wa Waislamu mkabala wa mashambulizi ya Marekani na Israel si jambo la kupuuzwa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141100-maulama_wa_pakistan_umoja_wa_waislamu_mkabala_wa_mashambulizi_ya_marekani_na_israel_si_jambo_la_kupuuzwa
Kongamano la kila mwaka lenye kaulimbiu ya “Kumpenda Mtume Mtukufu; Kitovu cha Umoja wa Waislamu” limefanyika mjini Islamabad Pakistan sambamba na maadhimisho ya kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Mtukufu wa Uislamu, Muhammad al-Mustafa (SAW), na Wiki ya Umoja.
(last modified 2026-08-31T16:54:26+00:00 )
Aug 31, 2026 11:13 UTC
  • Maulama wa Pakistan: Umoja wa Waislamu mkabala wa mashambulizi ya Marekani na Israel si jambo la kupuuzwa
    Maulama wa Pakistan: Umoja wa Waislamu mkabala wa mashambulizi ya Marekani na Israel si jambo la kupuuzwa

Kongamano la kila mwaka lenye kaulimbiu ya “Kumpenda Mtume Mtukufu; Kitovu cha Umoja wa Waislamu” limefanyika mjini Islamabad Pakistan sambamba na maadhimisho ya kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Mtukufu wa Uislamu, Muhammad al-Mustafa (SAW), na Wiki ya Umoja.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press kutoka Islamabad, wazungumzaji katika mkutano huo, wameashiria kuongezeka changamoto zinazoukabili Ulimwengu wa Kiislamu pamoja na hatua za Marekani na Israel katika eneo la Asia Magharibi na kusisitiza umuhimu wa kuweka kando tofauti za kimadhehebu na kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu.

Hafla hiyo iliandaliwa na Majlis-e-Wahdat-e-Muslimeen Pakistan chini ya usimamizi wa Baraza la Mshikamano wa Kitaifa la nchi hiyo. Viongozi kadhaa wa kisiasa na kidini, wanazuoni kutoka madhehebu mbalimbali pamoja na shakhsia wa kidini walihudhuria kongamano hilo.

Wazungumzaji katika kongamano hilo walisisitiza umuhimu wa kuweka kando tofauti za kimakundi na kimadhehebu na kuimarisha umoja wa Waislamu. Walieleza kuwa kumpena na kumfuata Mtume Muhammad (SAW) ni msingi wa pamoja unaoweza kuyakurubisha Pamoja makundi na madhehebu mbalimbali ya Kiislamu.

Aidha, walisisitiza umuhimu wa kudumisha uthabiti na mshikamano wa Pakistan na kukabiliana na njama ambazo, kwa mujibu wao, zinalenga kuleta mifarakano miongoni mwa Waislamu.

Allama Raja Nasir Abbas Jafari, mkuu wa Majlis-e-Wahdat-e-Muslimeen na kiongozi wa upinzani katika Baraza la Seneti la Pakistan, amesema kuwa Mtume Muhammad (SAW) alikuwa kielelezo cha maadili mema na utu. Alisema kwamba iwapo Waislamu wanajitambulisha kuwa wafuasi wa Mtume huyo, basi wanapaswa kueneza maadili mema na mwenendo mwema katika jamii.

Akizungumzia matukio ya eneo la Asia Magharibi, Allama Nasir Abbas amesema kuwa Marekani na Israel hazitaki kuiona Pakistan ikiwa nchi yenye nguvu na uthabiti, na kwamba njama za kuibua tofauti za ndani zinaweza kusababisha kudhoofika kwa nchi hiyo.