Malengo ya utawala wa Kizayuni ya kubakisha majeshi yake katika ardhi ya Syria
Asaad al-Shaibani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, amesisitiza kuwa tangazo la utawala wa Kizayuni kuhusu kuendelea kuwepo kwa majeshi yake katika ardhi ya Syria ni jaribio la kuimarisha na kudumisha uvamizi wake katika nchi hiyo.
Kufuatia kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad na kuundwa kwa serikali mpya nchini Syria, utawala wa Kizayuni umekiuka mara kwa mara mamlaka ya kujitawala nchi hiyo ya Kiarabu na huku ukidumisha mashambulizi dhidi ya nchi hiyo, umetuma majeshi yake katika maeneo mbalimbali nyeti ya Syria. Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, mashambulizi ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo yanaendelea; ambapo mashambulizi 65 ya aina hiyo yalirekodiwa mwezi Julai pekee, huku mengine 52 yakifanywa na majeshi ya Israel katika siku 18 za kwanza za mwezi Agosti. Swali linalojitokeza ni kuwa je, ni malengo gani yanafuatiliwa na utawala wa Kizayuni katika kuendeleza mashambulizi na kusisitiza uwepo wa vikosi vyake vya kijeshi ndani ya ardhi ya Syria?
Lengo kuu la utawala wa Kizayuni ni kukalia kwa mabavu ardhi ya Syria na hivyo kupanua zaidi ardhi za nchi za Kiarabu unazozikalia kwa mabavu. Kwa kuzingatia udhaifu wa serikali ya Syria na kutoweza kukabiliana na uvamizi wa utawala wa Kizayuni, utawala huo sasa imehamisha mbinu zake kutoka mapigano ya muda yanayohusiana na usalama hadi kuimarisha hali mpya ya eneo kusini mwa Syria. Ingawa Israel inahalalisha uwepo wake wa kijeshi katika sehemu za kusini mwa Syria kwa madai yasiyo na msingi, eti ya kulinda usalama wake, Damascus inasisitiza kwamba sisitizo la uwepo wa kudumu haliwezi kuzingatiwa tu kama hatua ya muda ya usalama; bali linapasa kutazamwa kama jaribio la kuanzisha ukweli mpya katika eneo. Lengo jingine la utawala wa Kizayuni ni kuunda "uhalisia mpya wa mambo ardhini" kabla ya kuelekea kwenye makubaliano ya kisiasa na serikali ya Syria. Kwa hakika, kwa kuimarisha uvamizi wake katika ardhi ya Syria, utawala huo unataka kubuni uhalisia mpya wa kiusalama kabla ya kufikia mazungumzo yoyote ya kisiasa, huku ukilenga kuingiza hali hiyo mpya katika makubaliano yatakayofikiwa wakati wa mazungumzo yanayoweza kufanyika hapo baadaye. Kwa kuzingatia mwelekeo wa utawala mpya wa Syria kuhusu makubaliano ya kisiasa na utawala wa Kizayuni, pamoja na utegemezi wake kwa Marekani, Tel Aviv inataka kutumia fursa hii kwa ajili ya kuendeleza uvamizi wa kudumu katika ardhi ya Syria na hata kuhalalisha uvamizi huo ndani ya vipengele vya makubaliano hayo.
Lengo jingine linalofuatiliwa na utawala wa Kizayuni ni kudhoofisha mamlaka ya kitaifa ya Syria. Mashambulio ya mara kwa mara na sisitizo la kuwepo kwa jeshi la Israel ndani ya ardhi ya Syria yanalenga kuhalalisha mwenendo huu wa utawala wa Kizayuni. Kwa kuzingatia udhaifu wa serikali iliyopo madarakani nchini Syria na kutoweza kwake kukabiliana na vitisho vya Tel Aviv, mamlaka ya kitaifa ya Syria itadhoofishwa zaidi, ambapo kwa hakika matokeo ya jambo hilo yanaendana na maslahi ya muda mrefu ya utawala wa Kizayuni.
Lengo jingine ni kuundwa kwa eneo la usalama (buffer zone) kusini mwa Syria. Ni wazi kuwa kama utawala wa Kizayuni utashindwa kuimarisha uvamizi wake katika ardhi ya Syria na kuiunganisha na ardhi nyingine za Waarabu zinazokaliwa kwa mabavu, angalau kupitia uvamizi wa mara kwa mara na uanzishwaji wa eneo la usalama, utahakikisha kuwa hakuna vikosi vyovyote vya jeshi la Syria vinavyoruhusiwa kupelekwa huko. Kwa kufanya hivyo, kimsingi Israel itakuwa imefanikiwa kuziweka ardhi hizo chini ya udhibiti wake wa kiintelijensia na kioperesheni.