Vita vya kidini vya utawala wa Kizayuni: Marufuku ya kutoa adhana katika Msikiti wa Ibrahimi yaingia siku ya 75
-
Vita vya kidini vya utawala wa Kizayuni: Marufuku ya kutoa adhana katika Msikiti wa Ibrahimi yaingia siku ya 75
Katika kipindi cha siku 75 zilizopita, utawala wa Kizayuni, pamoja na kukiuka heshima ya Msikiti wa Ibrahimi katika mji wa Al-Khalil, umekiuka waziwazi uhuru wa kidini wa Waislamu kwa kuzuia kutolewa adhana katika eneo hilo takatifu la Kiislamu.
Kwa mujibu wa Kituo cha Habari cha Palestina, Sheikh Mu’taz Abusnaina, Mkurugenzi wa Msikiti wa Ibrahimi, amesema kuwa uvamizi huo ni mwendelezo wa njama za adui wa Kizayuni za kubadilisha utambulisho wa kidini na kihistoria wa msikiti huo, na kulazimisha hali mpya ndani ya eneo hilo takatifu.
Amesema hatua hiyo pia ni mwendelezo wa sera ya utawala wa Israel ya kuwabana kwa makusudi waumini wa Kipalestina na kuwawekea vikwazo katika kutekeleza ibada zao.
Alikumbusha kwamba kuzuia kusikika sauti ya adhana na kuwabana waumini wa Kipalestina ni ukiukaji wa wazi wa uhuru wa kuabudu na hujumuisha kushambulia na kukiuka maeneo matakatifu ya Kiislamu.
Wizara ya Wakfu na Masuala ya Dini ya Palestina imesema katika taarifa yake kwamba, tangu tarehe 21 Juni iliyopita hadi sasa, utawala wa Kizayuni umezuia kutolewa adhana katika Msikiti wa Ibrahimi zaidi ya mara 350 kwa jumla.
Wizara ya Wakfu pia imeonya kuhusu kuongezeka hujuma dhidi ya Msikiti wa Ibrahim na wafanyakazi wake, na kusema kuwa kwa siku ya 20 mfululizo, mamlaka za utawala wa Kizayuni zimeendelea kumzuia Sheikh Mu’taz Abusnaina, Mkurugenzi wa Msikiti huo, pamoja na Humam Abumurkhia, Mkuu wa Wahudumu wa Msikiti huo, kuingia katika eneo hilo takatifu na kutekeleza majukumu yao.
Wizara hiyo imeitaka jamii ya kimataifa, mashirika yanayohusiana na Umoja wa Mataifa, pamoja na taasisi za haki za binadamu, kuingilia kati ili kusitisha mara moja hatua hizo na kuushinikiza utawala wa Kizayuni kukomesha uvamizi wake dhidi ya msikiti huo.