Yemen yaanzisha mashambulizi makubwa ya makombora na droni dhidi ya vituo vya mafuta vya Aramco, Saudia Arabia
-
Msemaji wa jeshi la Yemen, Yahya Saree
Jeshi la Yemen limeanzisha operesheni kubwa ya kijeshi inayolenga vituo vya mafuta vya Saudi Aramco na kambi za kijeshi za anga kusini mwa Saudi Arabia, ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi cha moja kwa moja dhidi ya kampeni ya kikatili ya mashambulizi ya anga ya siku tatu iliyofanywa na Riyadh, ambayo ilijumuisha mauaji ya kutisha katika gereza moja nchini Yemen.
Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumanne, msemaji wa jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree ameeleza kuwa makombora mengi ya balistiki na ndege zisizo na rubani (droni) yamepiga miundombinu ya kampuni ya Aramco katika miji ya Abha, Najran, na Jizan pamoja na kambi ya Jeshi la Anga la Saudia ya King Khalid katika mji wa Khamis Mushait.
Brigedia Jenerali Saree ameyataja mashambulizi hayo kuwa "sahihi na ya moja kwa moja," na kwamba yamesababisha uharibifu mkubwa kwa vituo vilivyokusudiwa.
Jeshi la Yemen limeshadidisha mashambulizi dhidi ya Riyadh kufuatia mashambulio 121 ya anga yaliyofanywa na Saudia katika muda wa saa 72 zilizopita katika mikoa kadhaa ya Yemen, ikiwemo Ma'rib, Al-Bayda, Al-Hudaydah, Taiz, na Al-Jawf.
Shambulio la kutisha zaidi kati ya hayo lililenga gereza kuu katika wilaya ya Al-Hazm, mkoani Al-Jawf.
Wizara ya Afya ya Umma na Idadi ya Watu ya Yemen imearifu kuwa shambulio hilo la anga lilijeruhi watu 14, saba waliuawa wakiwemo wafungwa sita na mtoto aliyekuwa amezuru gereza hilo, huku wengine saba wakijeruhiwa.
"Adui mtenda jinai Saudi Arabia ameanzisha uchokozi wa kikatili na usio wa haki dhidi ya Yemen... akitenda uhalifu mkubwa kwa kufanya mauaji ya halaiki huko Al-Jawf," ameeleza Msemaji wa jeshi la Yemen.