Baada ya kushtadi jinai za walowezi wa kizayuni, nchi 12 zatangaza marufuku ya biashara na vitongoji haramu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141312-baada_ya_kushtadi_jinai_za_walowezi_wa_kizayuni_nchi_12_zatangaza_marufuku_ya_biashara_na_vitongoji_haramu
Nchi 12 zimetoa taarifa ya pamoja zikitangaza marufuku ya kitaifa ya biashara kwa bidhaa zinazotoka kwenye vitongoji haramu vilivyojengwa na utawala wa kizayuni wa Israel katika maeneo ya Palestina ya Ukingo wa Magharibi unayoyakalia kwa mabavu.
(last modified 2026-10-14T04:35:26+00:00 )
Sep 09, 2026 03:10 UTC
  • Baada ya kushtadi jinai za walowezi wa kizayuni, nchi 12 zatangaza marufuku ya biashara na vitongoji haramu

Nchi 12 zimetoa taarifa ya pamoja zikitangaza marufuku ya kitaifa ya biashara kwa bidhaa zinazotoka kwenye vitongoji haramu vilivyojengwa na utawala wa kizayuni wa Israel katika maeneo ya Palestina ya Ukingo wa Magharibi unayoyakalia kwa mabavu.

Nchi hizo ni Ufaransa, Uingereza, Canada, Denmark, Uhispania, Finland, Ireland, Iceland, Norway, Poland, Ureno, na Sweden.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Waziri Mkuu wa Uingereza Andrew Burnham, na Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney wamesisitiza kwamba hali katika maeneo ya Palestina inazidi kuwa mbaya kutokana na vurugu "zisizo za kawaida" za walowezi na upanuzi wa vitongoji, wakisisitiza kwamba mradi mpya wa vitongoji "haukubaliki.

Viongozi hao wamepongeza hatua ambazo tayari zimechukuliwa na Ireland, Uhispania, Uholanzi, Norway, na Ubelgiji; na katika taarifa yao wameitaka Israel isimamishe mara moja upanuzi wa vitongoji, iwawajibishe walowezi wanaofanya vurugu, na kuchunguza madai ya uhalifu dhidi ya askari wake.

Aidha, ametangaza "upinzani wao thabiti kwa hatua yoyote ambayo itasababisha kunyakuliwa eneo la Palestina au kulazimishwa (Wapalestina) kuhama."

Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Ed Miliband, amesema: "Tutaweka vikwazo kwa makampuni na watu binafsi wanaosaidia kupanua vitongoji katika Ukingo wa Magharibi."

Katika taarifa ambayo haijawahi kutolewa hapo kabla, Miliband ameongezea kwa kusema: "Kile ambacho serikali ya Netanyahu inafanya huko Ghaza ni doa kwenye dhamiri ya ulimwengu na kuna ushahidi unaoongezeka kwamba uhalifu wa kivita umefanywa. Hali huko Palestina ni dharura ya kimaadili. Maangamizi ya kizazi dhidi ya Wapalestina katika sehemu za Ukingo wa Magharibi yanafanywa na "magaidi wa Israel," na serikali ya Israel mara nyingi imekuwa ikifumbia macho suala hili. Na baya zaidi, mawaziri wake wamekuwa wakitoa taarifa na kuchukua hatua za kuunga mkono kuhamishwa kwa nguvu Wapalestina. Hatutabaki bila kujali".

Katika kauli kali zaidi ya kulaani kuwahi kutolewa na serikali ya London, Miliband ametangaza kuwa, serikali hiyo imechukua msimamo rasmi kuhusu uvamizi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi, akiuita "haramu kabisa". Amesema: "Kukiri huku ni kwa kiwango kidogo zaidi kinachostahili kuonyeshwa kuhusiana na watu wanaoteseka na kinapaswa kiwe mwanzo wa kutekelezwa haki"…/