Ansarullah ya Yemen yaitaka Saudia ijiondoe kwenye gwanda na mwavuli wa Marekani na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141330-ansarullah_ya_yemen_yaitaka_saudia_ijiondoe_kwenye_gwanda_na_mwavuli_wa_marekani_na_israel
Harakati ya Ansarullah ya Yemen imeituhumu Saudi Arabia kuwa inatekeleza mipango ya Kizayuni katika eneo na kuwataka watawala wa Riyadh wajiondoe kwenye gwanda na mwavuli wa himaya ya Marekani na utawala wa Kizayuni.
(last modified 2026-09-09T12:28:34+00:00 )
Sep 09, 2026 11:42 UTC
  • Ansarullah ya Yemen yaitaka Saudia ijiondoe kwenye gwanda na mwavuli wa Marekani na Israel

Harakati ya Ansarullah ya Yemen imeituhumu Saudi Arabia kuwa inatekeleza mipango ya Kizayuni katika eneo na kuwataka watawala wa Riyadh wajiondoe kwenye gwanda na mwavuli wa himaya ya Marekani na utawala wa Kizayuni.

Sambamba na hayo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sana'a imesisitiza kujitolea na kushikamana Yemen kimisingi, kiitikadi, na kiendelevu na uungaji mkono wake kwa kadhia ya Palestina, likiwa ni suala kuu na la msingi la Umma wa Kiislamu.

Wizara hiyo imetoa taarifa na kutangaza kwamba: leo Yemen inalipia gharama ya msimamo wake huo thabiti na wa kiutu wa kuiunga mkono Palestina, na kuandamwa na mashambulio ya utawala wa Saudia.

Taarifa hiyo imesisitiza kwa kusema: kwa kiwango chochote kile ambacho adui Msaudi atajaribu kuitumbukiza Yemen kwenye migogoro na matatizo, hatafanikiwa kamwe kuikengeusha nchi hiyo na kuitoa kwenye mkondo wa kadhia yake kuu.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imesema: kuendelea uchokozi na mzingiro wa Saudia dhidi ya Yemen ni kumtumikia moja kwa moja adui Israel na kutoa pigo kwa lengo tukufu la ukombozi wa Palestina; na utawala wa Saudia umeonyesha kwa Umma wa Kiislamu kwamba ndiye mtekelezaji wa mipango na malengo ya Kizayuni ndani ya Yemen na katika eneo.

 

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Sana'a imemalizia kwa kutoa wito kwa utawala wa Saudia wa kuutaka ujiondoe kwenye gwanda na mwavuli wa Marekani na Israel, urejee kwenye mkondo sahihi, na kufanya haraka ya kulisaidia taifa la Palestina…/