Mkuu wa zamani wa Shin Bet: Kwa sasa tunaelekea kushuhudia mwisho wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141332-mkuu_wa_zamani_wa_shin_bet_kwa_sasa_tunaelekea_kushuhudia_mwisho_wa_israel
Mkuu wa zamani wa Shirika la Usalama wa Ndani la Israel Shin Bet amesema kuwa, vita vinavyoanzishwa na Tel Aviv havina lengo la kisiasa, na kwamba Israel inaelekea katika mwisho wa mradi wa Kizayuni.
(last modified 2026-09-10T02:47:29+00:00 )
Sep 10, 2026 02:45 UTC
  • Mkuu wa zamani wa Shin Bet: Kwa sasa tunaelekea kushuhudia mwisho wa Israel

Mkuu wa zamani wa Shirika la Usalama wa Ndani la Israel Shin Bet amesema kuwa, vita vinavyoanzishwa na Tel Aviv havina lengo la kisiasa, na kwamba Israel inaelekea katika mwisho wa mradi wa Kizayuni.

Ami Ayalon, mkuu wa zamani wa Idara ya Ujasusi wa Ndani ya utawala wa Kizayuni Shin Bet (Shabak), amekiri kwamba utawala huo haujafikia ushindi kamili katika vita vyake, kwa sababu Hamas na Hizbullah bado zinaendelea kufanya shughuli zao na zina uwezo wa kuitishia Tel Aviv.

Mkuu wa zamani wa Idara ya Ujasusi wa Ndani ya utawala wa Kizayuni, inalojulikana kama Shin Bet (Shabak) ameongeza kuwa, ukosefu wa malengo ya kisiasa katika vita ni miongoni mwa matatizo makubwa yanayoikabili Israel, na kwamba hatimaye hali hiyo haiwezi kupelekea ushindi.

Ayalon ameonya kwamba utawala wa Kizayuni umeshindwa katika mapambano ya kushawishi fikra za umma na kupata uhalali wa kimataifa, akisisitiza kuwa, nguvu za kijeshi pekee haziwezi kushinda fikra na itikadi.

Aliendelea kusema kuwa, kuendeleza vita bila kuweka dira au mtazamo wa kisiasa kwa ajili ya Wapalestina kunamaanisha kwamba Israel inaelekea katika mwisho wa mradi wa Kizayuni.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, maafisa na viongozi mbalimbali wa Israel wamekuwa wakikosoa vikali sera za Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na kuonya juu ya kusambaratika utawala huo ghasibu.

Meja Jenerali mstaafu wa Israel, Itzhak Brik, alionya Februari akitaja migawanyiko ya ndani, kutengwa kimataifa na kushindwa uongozi kama hatari za msingi.

Utafiti wa Jewish People Policy Institute uliripoti kuwa asilimia 55 ya Waisraeli wanaona mgawanyiko wa kisiasa na migogoro ya ndani kuwa tishio hatari zaidi kwa kuendelea kuwepo kwa utawala huo, huku asilimia 60 wakisema kuna hatari halisi ya vurugu za ndani.