Ripoti: Watu 8,000 wamekatwa viungo tangu kuanza kwa vita dhidi ya Gaza
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Quds (Qudsna), vyanzo vya Palestina vimeripoti kwamba tangu kuanza vita dhidi ya Gaza, visa 8,000 vya kukatwa viungo vya mwili vimeripotiwa. Aidha, katika hali ya sasa, watu 10,000 wenye ulemavu wa viungo wanahitaji huduma za urekebishaji na tiba ya viungo kwa dharura.
Wizara ya Afya ya Ukanda wa Gaza imetangaza kwamba, kutokana na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina, visa 8,000 vya kukatwa viungo vya mwili pamoja na visa 300 vya majeraha ya mfumo wa neva na uti wa mgongo vimesajiliwa katika eneo hilo.
Wizara ya Afya ya Ukanda wa Gaza imetangaza katika taarifa yake kwamba mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni tangu Oktoba 2023 yameacha janga kubwa la kibinadamu na kiafya ambalo halijawahi kushuhudiwa.
Wizara hiyo imesema kuwa, huduma za tiba ya viungo na urekebishaji wa afya (physiotherapy and medical rehabilitation services) huko Gaza zimebadilika kutoka kuwa huduma ya ziada na kuwa muhimu kwa ajili ya kuokoa maisha na kuendeleza matibabu. Kwa sasa, huduma hizo zimekuwa mstari wa mbele katika kuzuia ulemavu wa kudumu miongoni mwa maelfu ya watu waliojeruhiwa na kuathirika na vita vya kinyama vya utawala ghasibu wa Israel.
Mkuu wa Hospitali ya Hamad ya Urekebishaji na Viungo Bandia (Prosthetics) katika Ukanda wa Gaza ameziambia duru za habari kwamba, idadi ya watu waliokatwa viungo kutokana na vita vya Gaza imepindukia 8,000, wakiwemo baadhi ya wanawake na watoto. Takwimu hiyo inaonesha ukubwa wa janga la kiafya na kibinadamu linaloendelea katika Ukanda wa Gaza.