Yemen yashambulia kambi ya kijeshi ya Saudia kwa makombora na ndege zisizo na rubani kulipiza kisasi
-
Msemaji Mkuu wa Majeshi ya Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree
Majeshi ya Jamhuri ya Yemen (YAF) yametekeleza operesheni kubwa ya pamoja ya makombora ya balistiki na ndege zisizo na rubani (droni) dhidi ya kambi ya kijeshi ya Saudia katika eneo la Sharurah mkoani Najran kusini mwa ufalme huo, ikiwa ni jibu kwa kuendelea mashambulizi ya Saudia dhidi ya ardhi ya Yemen.
Msemaji Mkuu wa Majeshi ya Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree, amebainisha kuwa mashambulizi hayo yalilenga maghala ya silaha pamoja na vyumba vya amri na udhibiti vinavyotumika kuratibu na kuendesha uchokozi wa kijeshi dhidi ya Yemen na wananchi wake.
Amesema: “Operesheni hiyo ilitekelezwa kwa makombora ya balistiki na ndege zisizo na rubani, na shabaha zimelengwa kwa usahihi wa hali ya juu na moja kwa moja.”
Brigedia Jenerali Saree pia ameonya kuwa kuendelea kwa mashambulizi ya Saudia kutakabiliwa na mapigo makubwa zaidi ya kulipiza kisasi kutoka kwa majeshi ya Yemen.
Tamko hilo lilifuatia onyo alilolitoa Saree mapema Jumamosi akisisitiza kuwa jinai na hujuma za Saudia dhidi ya Yemen hazitapita bila kujibiwa. Alieleza kuwa ndege za kivita za Saudia zilikuwa zimetekeleza mashambulizi 129 katika majimbo saba ya Yemen ndani ya saa 48 zilizopita.
Matukio haya yanajiri huku kukiwa na mafanikio na kusonga mbele kusikokuwa na kifani kwa Majeshi ya Yemen dhidi ya mamluki wanaoungwa mkono na muungano unaoongozwa na Saudia kwenye pwani ya magharibi ya Yemen.
Kamanda mwandamizi wa kijeshi wa Yemen amesema kuwa vikosi vyao vimetoa pigo zito dhidi ya mpango wa kibeberu wa “Mashariki ya Kati Mpya” baada ya kukamilisha udhibiti wao kamili juu ya Lango-Bahari la kimkakati wa Bab al-Mandab.
Majeshi ya Yemen yamethibitisha ukombozi na udhibiti wa Kisiwa cha Perim (kinachojulikana pia kama Kisiwa cha Mayyun kwa Kiarabu). Kisiwa hiki kinapatikana ndani ya Lango-Bahari la Bab al-Mandab, ambalo linaunganisha Bahari ya Sham na Ghuba ya Aden.
Kusonga mbele huko kulifuatia kukombolewa mji wa pwani ya magharibi wa Mokha siku ya Alhamisi, hatua iliyoyalazimu majeshi ya mamluki wanaofadhiliwa na Saudia kurudi nyuma kuelekea kusini katika eneo la Dhubab.
Yemen imeapa kuendelea na operesheni zake za kujibu mapigo hadi Saudia itakapositisha vita vyake vya uchokozi vya muda mrefu pamoja na mzingiro haramu na wa kidhalimu dhidi ya taifa hilo.