Yemen yashambulia maegesho ya ndege za kivita, rada na maghala ya silaha ya kituo cha anga cha Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141464-yemen_yashambulia_maegesho_ya_ndege_za_kivita_rada_na_maghala_ya_silaha_ya_kituo_cha_anga_cha_saudia
Vikosi vya Jeshi la Yemen vimefanya shambulio la pamoja la makombora na ndege zisizo na rubani kwenye kambi kubwa ya anga katika eneo la kusini mwa Saudi Arabia la Asir kulipiza kisasi kwa shambulio la hivi karibuni la uchokozi wa kijeshi lililofanywa na Saudia na mzingiro inaoendelea kuiwekea nchi hiyo.
(last modified 2026-09-15T04:06:14+00:00 )
Sep 15, 2026 04:04 UTC
  • Ndege za kivita za Saudia
    Ndege za kivita za Saudia

Vikosi vya Jeshi la Yemen vimefanya shambulio la pamoja la makombora na ndege zisizo na rubani kwenye kambi kubwa ya anga katika eneo la kusini mwa Saudi Arabia la Asir kulipiza kisasi kwa shambulio la hivi karibuni la uchokozi wa kijeshi lililofanywa na Saudia na mzingiro inaoendelea kuiwekea nchi hiyo.

Msemaji wa jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree, ametangaza katika taarifa iliyorushwa hewani kwenye televisheni siku ya Jumatatu kwamba vitengo vya jeshi la nchi hiyo vimefanya operesheni kubwa na makini dhidi ya Kambi ya Anga ya Mfalme Khalid karibu na mji wa Saudia wa Khamis Mushait, ulioko kilomita zipatazo 884 kusini mwa mji mkuu Riyadh.

Amebainisha kuwa makombora mengi ya balestiki ya Yemen yaliyotengenezwa ndani ya nchi na ndege zisizo na rubani za kivita yalipiga mitambo ya kijeshi na miundombinu, maegesho ya ndege za kivita, mifumo ya rada, njia za kurukia ndege, vituo vya silaha, na maeneo mengine yaliyokusudiwa kulengwa ndani ya kambi hiyo ya anga.

"Vikosi vya Jeshi la Yemen vitaendeleza operesheni zao za kijeshi zenye umakini mkubwa ndani kabisa ya Saudi Arabia madamu uchokozi wa wazi dhidi ya watu wetu unaendelea. Uchokozi wowote mpya utajibiwa kwa hatua madhubuti na kali zaidi," amesisitiza Saree.

Afisa huyo mwandamizi wa Yemen ameongezea kwa kusema, "Tutaendelea kushikilia msimamo wa kulipiza kisasi kwa hatua sawia—kwa kujibu mzingiro kwa mzingiro na kushadidisha mashambulizi ya kijeshi pale upande wa pili utapotangulia kufanya hivyo—na tutalenga mikusanyiko ya askari wa Saudia hadi pale uchokozi utakapokoma na mzingiro dhidi ya nchi yetu azizi utakapoondolewa kikamilifu."

Mnamo Julai 20, serikali ya Sana'a ilitangaza mzingiro wa baharini dhidi ya Saudi Arabia likiwa ni jibu kwa "mzingiro usio wa haki na wa kidhalimu" uliowekwa dhidi ya Yemen na kudumu kwa takriban miaka 12.

Kufuatia hatua hiyo, vikosi vya jeshi la Yemen vimeripoti mfululizo wa operesheni za mashambulizi zilizofanyika kwa mafanikio kulenga meli zenye uhusiano na Saudi Arabia katika Bahari Nyekundu…/