Waandishi wa habari 37 Wapalestina wanashikiliwa kwenye jela za Israel, 19 bila kufunguliwa mashtaka
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141466-waandishi_wa_habari_37_wapalestina_wanashikiliwa_kwenye_jela_za_israel_19_bila_kufunguliwa_mashtaka
Utawala wa kizayuni wa Israel unawashikilia waandishi wa habari 37 wa Kipalestina katika magereza yake, wakiwemo 19 waliowekwa kwenye kizuizi kisicho na kikomo kwa kutumia sheria ya kutofunguliwa mashtaka au kutofikishwa mahakamani. Hayo yameelezwa katika taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Wafungwa wa Kipalestina, Palestinian Prisoner Society.
(last modified 2026-09-15T04:12:37+00:00 )
Sep 15, 2026 04:06 UTC
  • Waandishi wa habari 37 Wapalestina wanashikiliwa kwenye jela za Israel, 19 bila kufunguliwa mashtaka

Utawala wa kizayuni wa Israel unawashikilia waandishi wa habari 37 wa Kipalestina katika magereza yake, wakiwemo 19 waliowekwa kwenye kizuizi kisicho na kikomo kwa kutumia sheria ya kutofunguliwa mashtaka au kutofikishwa mahakamani. Hayo yameelezwa katika taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Wafungwa wa Kipalestina, Palestinian Prisoner Society.

Taasisi hiyo isiyo ya kiserikali imesema, waandishi hao wote 37 walikamatwa na kuwekwa kizuizini kufuatia kuanza kwa mauaji ya kimbari ya Ghaza mnamo Oktoba 2023.

Taarifa ya Jumuiya ya Wafungwa wa Kipalestina imesema, utawala wa kizayuni unaendelea kuwalenga waandishi wa habari wa Kipalestina kupitia utiaji nguvuni, hukumu za vifungo jela, kifungo cha upweke na kuwafungulia mashtaka kwa sababu ya kazi yao na kutumia uhuru wa kutoa maoni.

Miongoni mwa waliokamatawa na kuwekwa kizuizini hivi karibuni ni waandishi wa habari Muath Ammarna na Sabri Jibrin, ambao walikamatwa siku ya Alkhamisi iliyopita baada ya vikosi vya Israel kuvamia nyumba zao huko Bethlehemu kusini mwa Ukingo wa Magharibi.

Jumuiya hiyo imeendelea kueleza katika taarifa yake kwamba, waandishi wa habari walioko kizuizini wanakabiliwa na mazingira sawa na waliyonayo wafungwa wengine Wapalestina ya kuwekwa na njaa, kukosa huduma za matibabu, kuteswa, kuwekwa kiupweke na kunyimwa haki za msingi.

Wanahabari Wapalestina hulengwa pia na mamlaka za utawala wa kizayuni wa Israel kupitia mauaji, kulazimishwa kutoweka na kufikwa na mashambulizi ya moja kwa moja wakati wa ufanyaji kazi zao, imeongeza taarifa hiyo, na kufafanua kwamba, hiyo ni sehemu ya sera ya kimfumo inayolenga kuzuia kuripotiwa na kuandikwa na Wapalestina uhalifu na ukiukaji wa sheria unaofanywa na utawala wa kizayuni wa Israel.

Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu unashuhudia uvamizi wa jeshi la Israel kila siku na mashambulizi yanayoongezeka tangu yalipoanza mauaji ya kimbari ya Ghaza Oktoba 2023. Mashambulizi hayo yamejumuisha mauaji, ukamataji watu, ubomoaji wa majengo, mashambulizi dhidi ya nyumba, magari na misikiti, uharibifu wa ardhi za kilimo, kuwawekea vizuizi wakulima, kuwahamisha Wapalestina katika makazi yao na kupanua vitongoji haramu…/