Watengezaji wa filamu NAZA iliyofichua ukweli wa mauaji ya kimbari ya Ghaza hatarini kuvuliwa uraia wa Israel
Waziri wa Utamaduni wa utawala wa kizayuni wa Israel, Miki Zohar amesema atajaribu kuhakikisha watengenezaji wa filamu iitwayo NAZA inayofichua "mfumo wa mauaji" uliotumiwa dhidi ya raia wa Palestina huko Ghaza wakati wa mauaji ya kimbari yaliyofanywa na utawala huo wa kizayuni wanavuliwa uraia wao kwa kufanya "uhaini".
Zohar amedai kuwa NAZA ni filamu ya "kuchukiza" na kwamba kushinda kwake Tuzo Maalumu ya Jopo la Majaji katika Tamasha la 83 la Kimataifa la Filamu la Venice siku ya Jumamosi iliyopita lilikuwa jambo la "kushtusha".
"Chuki kali za kuunguza walizonazo watengenezaji hao dhidi yao wenyewe, na dhamira yao ya kulidhuru taifa lao kwa ajili ya kupata sifa kutoka kwa watu wenye chuki dhidi ya Wayahudi kote duniani, ni jambo lisiloeleweka na linachukuliwa kuwa ni usaliti dhidi ya taifa," amedai waziri huyo wa utawala wa kizayuni katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa X.
"Nitachukua hatua mara moja kufuta uraia wa Israel wa watengenezaji hawa wa filamu wanaochukiza, kwa sababu za uhaini dhidi ya taifa," ameongezea kueleza Zohar.
Filamu NAZA, iliyoongozwa na watengenezaji filamu walioshinda tuzo ya Oscar, Yuval Abraham na Rachel Szor, inachunguza mifumo iliyotumika katika mauaji ya halaiki ya kukusudia yaliyofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya raia madhulumu wa Palestina wa Ukanda wa Ghaza.
Filamu hiyo ya matukio halisi, yaani Documentary, inaakisi mahojiano waliyofanyiwa watu 24 wa ndani ya jeshi na idara ya ujasusi ya Israel ambao utambulisho wao umefichwa.
Waisraeli hao wanaelezea matumizi ya mifumo inayotumia akili bandia (AI) ambayo jeshi la kizayuni liliitumia kubaini shabaha na kufanya mashambulizi ya mabomu kutokea mbali, huku mara nyingi likijua kwamba idadi kubwa ya raia wangeuawa.
Mmoja wa watu wa ndani ya jeshi waliohojiwa kwa ajili ya filamu hiyo alisema, katika tukio moja, ilitolewa ruhusa ya kuua hadi raia 500 Wapalestina kwa ajili ya kumpata mwanachama mmoja tu muhimu wa harakati ya Palestina ya Hamas.
Filamu NAZA ilipata sifa kemkemu katika Tamasha la Kimataifa la Filamu la Venice, ikiwemo ya kuvunja rekodi kwa kushangiliwa kwa kusimama na hadhira kwa muda wa dakika 24.5 wakati wa onyesho lake la kwanza mnamo tarehe 10 Septemba…/