Umoja wa Mataifa wataka wakaguzi wa kimataifa waruhusiwe kufika maeneo yote ya Gaza
Umoja wa Mataifa umeashiria kugunduliwa mamia ya miili chini ya vifusi katika Ukanda wa Gaza na kutoa wito wakaguzi wa kimataifa waruhusiwe kuingia na kufika katika maeneo yote ya ukanda huo ili kukusanya ushahidi na kuchunguza uwezekano wa kutendeka uhalifu wa kivita.
Volker Türk Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu amesema, kugunduliwa mabaki mengi ya binadamu, ambayo kwa kiasi kikubwa ni ya wanawake na watoto, chini ya vifusi vya majengo yaliyoharibiwa huko Gaza, kumeongeza wasiwasi kuhusu uwezekano wa kutendeka uhalifu wa kivita.
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema, ulinzi wa raia wa Palestina hadi sasa umefanikiwa kutoa zaidi ya miili 630 na mabaki ya binadamu kutoka chini ya vifusi vya majengo yaliyobomolewa, huku idadi ya watu wanaodhaniwa kuwa wamepotea na kubaki chini ya vifusi ikikadiriwa kuwa zaidi ya 8,000.
Türk ametaka waathiriwa waandikwe na kutambuliwa, ushahidi wa kitabibu na wa kiuchunguzi pamoja na sampuli za kibaolojia zihifadhiwe, na familia za waathiriwa zijulishwe. Aidha, amesisitiza kuwa wakaguzi wa kimataifa wanapaswa kupewa fursa ya kufikia maeneo yote ya Gaza.
Katika upande mwingine Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena umesema una wasi wasi mkubwa juu ya hali mbaya sana ya maisha katika Ukanda wa Gaza sambamba na kushadidi mashambulizi ya mabomu na makombora yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina wa eneo hilo lililowekewa mzingiro.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na la Afya Duniani (WHO) yameonya kuhusu kuzorota hali ya kibinadamu katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kimabavu na Israel.
Ripoti zinaonyesha kuwa, theluthi mbili ya wakazi wa Gaza bado wanakabiliwa na viwango vya dharura vya njaa, na bila kuongezeka msaada wa kibinadamu, hadi asilimia 90 ya wakazi wanaweza kukabiliwa na viwango vya juu vya ukosefu mkali wa chakula kabla ya mwisho wa mwaka huu.