Saudia yafungua anga yake kwa ndege zinazoenda Israel
Kwa mara ya kwanza, Saudi Arabia imefungua anga yake na kuziruhusu ndege za shirika la Air India kutumia anga hiyo katika safari zake za kwenda na kutoka Israel.
Katika hatua hiyo ambayo kwa mara nyingine tena inadhihirisha jitihada za utawala wa Al-Saud na utawala wa Kizayuni wa Israel za kuimarisha uhusiano wa pande mbili, ndege ya abiria ya India Air jana usiku kwa mara ya kwanza kabisa ilipitia Saudia kabla ya kuendelea na safari hadi Tel Aviv.
Praveen Bhatnagar, msemaji wa shirika hilo la ndege la India amesema ndege zao kuanzia jana zilianza kusafiri kutoka New Delhi hadi Tel Aviv zikitumia anga ya Saudia.
Waziri wa Uchukuzi wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Yisrael Katz, amesema hatua ya ndege za abiria kuruhusiwa rasmi kuunganisha safari zake kutoka Riyadh hadi Tel Aviv ni ya kihistoria na ambayo haijawahi kutokea.
Mapema mwaka huu, gazeti la Basler Zeitung linalochapishwa kwa lugha ya Kijerumani nchini Uswisi lilifichua mpango wa Saudi Arabia kutaka kununua mfumo wa ngao ya makombora kutoka utawala wa Kizayuni wa Israel, wiki chache baada ya gazeti moja la Kizayuni kufichua kuwa, katika mkataba wa mabilioni ya dola wa ununuzi silaha baina ya Marekani na Saudia, baadhi ya mashirika ya uundaji silaha ya Israel yalianishwa kuwa yangestafidi na makubaliano hayo.
Hivi karibuni pia afisa mmoja wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambaye hakutaka jina lake litajwe alifichua kuwa Muhammad bin Salman Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia mwezi Septemba mwaka jana alifanya safari za siri huko Israel ambapo alikutana na viongozi wa ngazi za juu wa utawala huo.