Arubaini ya Imam Husain AS, nembo ya umoja baina ya Iran na Iraq
Maandamano ya mamilioni ya watu katika Arubaini ya Imam Husain AS na wajibu wa kuimarishwa kadiri inavyowezekana uhusiano wa Tehran na Baghdad ndiyo ajenda kuu ya mazungumzo ya simu yaliyofanywa baina ya mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Iraq.
Jana Alkhamisi jioni, Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alizungumza kwa simu na Muhammad Ali al Hakim, waziri mpya wa mambo ya nje wa Iraq ambapo sambamba na kumpongeza kwa kuchaguliwa kuwa waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo alisema kuwa ana matumaini uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi hizi mbili jirani utazidi kuimarika katika nyuga zote.

Baada ya kumpa pongezi hizo, Zarif alizungumzia suala la kidini la maadhimisho ya mamilioni ya watu ya Arubaini ya Imam Husain AS na kusema kuwa: Maandamano ya Arubaini ya Imam Husain AS ni nembo ya adhama na heshimu kubwa waliyo nayo watu wa nyumba takatifu ya Bwana Mtume Muhammad SAW kama ambavyo pia ni nembo ya ushirikiano, mshikamano na umoja baina ya mataifa haya mawili ndugu.
Kwa upande wake, waziri mpya wa mambo ya nje wa Iraq, Muhammad Ali al Hakim amegusia uhusiano mzuri na wa kihistoria wa mataifa mawili ya Kiislamu ya Iran na Iraq na kusisitizia wajibu wa kustawishwa uhusiano wa mataifa hayo mawili ndugu kadiri inavyowezekana.
Vile vile amesema kuwa wafanyaziara ya Arubaini ya Imam Husain AS ni wageni azizi wa serikali na taifa la Iraq na amemuhakikishia waziri wa mambo ya nje wa Iran kuwa juhudi za kila upande zimefanyika na zinaendelea kufanyika kwa ajili ya kuwarahisishia safari za maeneo yote matakatifu wafanyaziara hao. Iran na Iraq ni majirani wawili ambao wana mambo mengi sana ya kuwaunganisha na moja ya dhihirisho la wazi kabisa la ushirikiano huo ni umoja na mshikamano unaoonekana kwenye maadhimisho ya Arubaini ya Imam Husain AS. Kila mwaka maadhimisho hayo yanazidi kuimarisha ushirikiano, urafiki na kushibana mataifa mawili ya Iran na Iraq na kuchora picha nzuri ya kuishi pamoja kiudugu na kimapenzi. Lugha, utamaduni, madhehebu na dini moja ni katika mambo yanayoyakutanisha mataifa mawili ya Iran na Iraq kwenye mambo mengi na hata tunaweza kusema kuwa mambo hayo ya pamoja ni jiwe la msingi la kuweko uhusiano mzuri na wa kiistratijia baina ya Tehran na Baghdad.

Mapokezi mazuri sana na yaliyojaa mapenzi ya wananchi wa Iraq kwa wafanyaziara ya Arubaini ya Imam Husain AS ni dhihirisho la wazi la umoja wa Kiislamu katika upeo wake mpana na hili ndilo jambo ambalo linaufanya uhusiano wa mataifa haya mawili ya Iran na Iraq uwe wa kipekee kabisa.
Maandamano ya mamilioni ya Waislamu kwa ajili ya Arubaini ya Imam Husain AS yanaongeza maradufu umuhimu wa uhusiano wa Iran na Iraq na ni kwa kutumia fursa hiyo ndio maana nchi hizo mbili zimetiliana saini hati ya maelewano yenye vifungu 9 na vipengee 71. Usalama wa wafanyaziara ya Arubaini ya Imam Husain AS na namna ya kushirikiana taasisi husika katika jambo hilo, ni moja ya vipengee vya hati hiyo ya maelewano.
Abbas Salehi, Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu wa Iran alisema siku ya Alkhamisi kwamba: Maadhimisho ya Arubaini ya Imam Husain AS ni dhihirisho maalumu la nguvu za Waislamu wa Kishia duniani na kuna wajibu wa kufanyika juhudi kubwa zaidi za kuionesha hamasa hiyo ya Arubaini ya Imam Husain AS kwa sura pana na bora zaidi kwa walimwengu wote.

Naye Iraj Masjedi, balozi wa wa Iran nchini Iraq amesema: Kushiriki mamilioni ya wananchi wa Iran bega kwa bega na mamilioni mengine ya wapenzi wa Ahulul Bayt watoharifu AS kutoka kila kona ya dunia katika mjumuiko wa mamilioni ya watu kwa ajili ya kuadhimisha Arubaini ya Imam Husain AS, kunazidi kutia nguvu na kuimarisha uhusiano wa kidugu na kirafiki baina ya wapenzi wa Watu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW hususan baina ya wananchi wa Iran na Iraq.
Kufanyika maadhimisho hayo katika mazingira mazuri ya utulivu na usalama mkubwa kunaonesha umuhimu wa uhusiano wa kiistratijia baina ya Iran na Iraq na kwamba ni chini ya kivuli cha uhusiano huo ndipo zilipoweza kuvunjwa na kusambaratishwa njama za kigaidi za Daesh (ISIS) huko Iraq na kuleta usalama na amani yenye kutia matumaini nchini humo.