Rais Bashar al Assad: Mapambano dhidi ya magaidi ni utangulizi wa mapambano dhidi ya Marekani
Rais Bashar al Assad wa Syria amesema kuwa mapambano dhidi ya magaidi ni utangulizi wa makabiliano ya uwepo haramu wa askari wa Marekani nchini humo.
Rais Assad ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Phoenix ya China ambayo yamerushwa hewani leo na kubainisha kwamba, makabiliano ya jeshi la Syria dhidi ya magaidi, yamedhoofisha uwepo wa Marekani nchini humo kama ambavyo pia yameyalemaza makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Washington nchini Syria. Amesema kuwa kwa juhudi za serikali ya Damascus, maeneo yote ya nchi hiyo yatakombolewa kutoka mikononi mwa magenge ya kigaidi. Akibainisha kwamba Marekani inapora mafuta ya Syria na kuyauza kwa Uturuki, Rais Bashar al Assad amesema kuwa, tangu awali Uturuki ilikuwa ikishiriki kuuza moja kwa moja mafuta ya nchi hiyo yaliyoporwa kutoka Syria kwa kushirikiana na makundi ya kigaidi kama vile Jab'hatu Nusra na Daesh (ISIS) na kwamba hii leo pia Ankara ingali inashirikiana na Marekani katika suala hilo.
Ameashiria mpango unaoitwa 'Belt and Road' wa China ambao una lengo la kuleta mabadiliko katika ngazi ya uhusiano wa kimataifa na kusema, mpango huo umeratibiwa kwa lengo la kuleta ushirikiano kwa maslahi ya pamoja badala ya njama za ubeberu. Aidha amekaribisha uwekezaji wa mashirika ya China katika soko la Syria na kuongeza kuwa, serikali ya Beijing iliwasilisha pendekezo la misaada kwa Syria katika uga wa ukarabati ambapo pia kulifanyika mazungumzo mengi na mashirika kadhaa ya China kwa ajili ya kufidia hasara zinazotokana na vikwazo.