Bashar al-Assad kuwania tena urais Syria katika uchaguzi wa mwezi ujao
Rais Bashar al-Assad wa Syria leo amekabidhi fomu za kugombea kiti cha urais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika tarehe 26 ya mwezi ujao wa Mei.
Hayo yameelezwa na Hammouda Youssef Sabbagh, Spika wa Bunge la Syria katika mkutano wake na waandishi wa habari. Rais Assad anawania kuiongoza Syria kwa muhula wa tatu ambapo katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, serikali yake imekumbwa na misukosuko na njama za madola ya kigeni yaliyotaka kumuondoa madarakani.
Rais Bashar al-Assad (55) aliibuka mshindi kwa kujipatia asilimia 88 ya kura katika uchaguzi uliopita wa urais uliofanyika mwaka 2014.
Syria inajiandaa kwa uchaguzi wa Mei 26 mwaka huu huku zoezi la wagombea kujiandikisha likiendelea katika hali ambayo, taifa hilo la Kiarabu limekuwa likiandamwa na mapigano, hujuma za kigaidi na uingilaji wa kigeni kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.
Kwa mujibu wa Spika wa Bunge la Syria, miongoni mwa masharti kwa wagombea wa urais katika uchaguzi huo wa mwezi ujao, ni kwamba lazima wawe wameishi nchini Syria kwa muda wa miaka kumi mfululizo, sambamba na kuwa na uungaji mkono wa angalau wabunge 35.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa, kufanyika uchaguzi huo wa rais kutakuwa ni ushindi mwingine kwa taifa hilo na itakuwa sababu ya kupungua uingilaji wa kigeni kama ambavyo hilo litaongeza kasi ya mchakato wa kuijenga upya nchi hiyo ya Kiarabu.