Rais Assad wa Syria aalikwa kuhudhuria kikao cha Baghdad cha viongozi wa nchi za eneo
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i73582-rais_assad_wa_syria_aalikwa_kuhudhuria_kikao_cha_baghdad_cha_viongozi_wa_nchi_za_eneo
Duru za habari zimeripoti kuwa serikali ya Iraq imemwalika rais wa Syria kushiriki katika kikao cha viongozi wa nchi jirani na Iraq kitakachofanyika mjini Baghdad.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 16, 2021 08:04 UTC
  • Rais Assad wa Syria aalikwa kuhudhuria kikao cha Baghdad cha viongozi wa nchi za eneo

Duru za habari zimeripoti kuwa serikali ya Iraq imemwalika rais wa Syria kushiriki katika kikao cha viongozi wa nchi jirani na Iraq kitakachofanyika mjini Baghdad.

Televisheni ya Al Mayadin imeripoti kuwa, katika safari yake mjini Damascus, Falih al Fayyadh, kiongozi wa Al-Hashdu-Sha'abi ya Iraq amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Bashar al Assad wa Syria.

Kwa mujibu wa ripoti ya Al Mayadin, katika mazungumzo hayo, Al Fayadh alimkabidhi Assad barua ya mwaliko kutoka serikali ya Iraq wa kushiriki kikao cha viongozi wa nchi jirani na Iraq kitakachofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Baghdad.

Mnamo mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti, na kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1990, Iraq itaitisha mkutano utakaohudhuriwa na karibu nchi 10 za Kiarabu, za kikanda na za Ulaya, zikiwemo nchi tano zinazopakana nayo, ambazo ni Iran, Uturuki, Saudi Arabia, Kuwait na Jordan.

Hadi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Saudi Arabia na Misri zimeshapewa mwaliko wa kushiriki katika kikao hicho; na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, naye pia ametangaza utayari wake wa kuhudhuria kikao hicho cha Baghdad.../