Rais wa Syria asifu na kupongeza sera na misimamo ya Oman kuhusiana na nchi yake
Rais Bashar al Assad wa Syria ameipongeza Oman kutokana na nafasi yake kuu na yenye mlingano kuhusiana na nchi yake.
Rais wa Syria ameyasema hayo katika mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Oman Badr bin Hamad Al-Busaidi pamoja na ujumbe alioandamana nao ambapo pande hizo mbili zimejadili na kubadilishana mawazo kuhusu uhusiano wa kipekee na wa aina yake uliopo kati ya Muscat na Damascus katika nyanja za ushirikiano wa pande mbili.
Kustawishwa na kuimarishwa uhusiano wa Oman na Syria na vilevile matukio ya kikanda na ya nchi za Kiarabu pamoja na kadhia za pamoja zinazopewa umuhimu na nchi mbili, ni maudhui nyingine zilizotawala mazungumzo kati ya Rais Assad na Hamad Al-Busaidi.
Katika mazungumzo hayo, Rais wa Syria ameashiria muelekeo na nafasi yenye mlingano ya Oman na sera na misimamo yake kuhusiana na Syria na uungaji mkono wa nchi hiyo na watu wake kwa serikali na wananchi wa Syria katika vita vya kupambana na ugaidi.
Kwa upande wake, Badr bin Hamad Al-Busaidi amewasilisha kwa rais wa Syria salamu za Sultan Haitham bin Tariq wa Oman na sisitizo lake juu ya misimamo thabiti ya nchi hiyo kuhusiana na Syria na akaeleza kwamba, Syria ni nguzo kuu katika Ulimwengu wa Waarabu na kwamba sera na misimamo imara na ya kishujaa ya Damasacus ni mwega unaoweza kutegemewa sana katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizouzunguka ulimwengu huo.../