Zaidi ya dazeni mbili za vyama vya Kiarabu vyataka kuondolewa haraka vikwazo dhidi ya Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i94170-zaidi_ya_dazeni_mbili_za_vyama_vya_kiarabu_vyataka_kuondolewa_haraka_vikwazo_dhidi_ya_syria
Zaidi ya dazeni mbili za vyama vya siasa vya Kiarabu vimetaka kuondolewa haraka vikwazo vyote vilivyowekwa na Marekani na washirika wake wa Magharibi dhidi ya Syria, hususan baada ya tetemeko kubwa la ardhi la 7.8 kwa kipimo cha Rishta lililoathiri maeneo ya kaskazini mwa Syria na nchi jirani ya Uturuki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 18, 2023 00:02 UTC
  • Zaidi ya dazeni mbili za vyama vya Kiarabu vyataka kuondolewa haraka vikwazo dhidi ya Syria

Zaidi ya dazeni mbili za vyama vya siasa vya Kiarabu vimetaka kuondolewa haraka vikwazo vyote vilivyowekwa na Marekani na washirika wake wa Magharibi dhidi ya Syria, hususan baada ya tetemeko kubwa la ardhi la 7.8 kwa kipimo cha Rishta lililoathiri maeneo ya kaskazini mwa Syria na nchi jirani ya Uturuki.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na vyama 26 vya siasa vya Kiarabu, imetaka kukomeshwa hatua za upande mmoja dhidi ya Syria na kueleza mshikamano wao na uongozi na taifa hilo.

Taarifa ya vyama hivyo imesema: "Tunalaani na kukemea vikali hatua zote za kiholela zinazochukuliwa na Marekani na washirika wake dhidi ya taifa la Kiarabu la Syria."

Vyama hivyo pia vimetoa wito kwa Umoja wa Mataifa na mashirika husika ya kimataifa kuchukua hatua za haraka zinazolenga kuondoa vikwazo na kuwasilisha misaada muhimu ya kibinadamu katika maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko la ardhi nchini Syria.

Wakati huo huo, Rais wa Syria Bashar al-Assad amezishukuru nchi na mataifa rafiki kwa msaada wao kufuatia tukio hilo la kusikitisha akisisitiza kuwa kiwango cha maafa haya ni kikubwa zaidi ya uwezo wa Syria.

Rais wa Syria amesema, raia wa kigeni na Wasyria wanaoishi ng'ambo wamejaribu kwa kila njia kuvunja mzingiro wa nchi za Magharibi dhidi ya nchi hiyo na kuwasaidia ndugu zao walioathiriwa na tetemeko la ardhi kadiri walivyoweza.

Assad

Hapo awali, katika taarifa yake ya kwanza kwenye televisheni ya taifa baada ya tetemeko la ardhi, Assad aliwaambia waandishi wa habari alipokuwa akitembelea maeneo yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi kwamba: Nchi za Magharibi hazijali hali ya binadamu.

Ikumbukwe kuwa Februari sita mitetemeko miwili mikubwa ya ardhi yenye ukubwa wa 7.8 na 7.5 kwa kipimo cha Rishta iliyakumba maeneo ya kusini mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria. Hadi sasa karibu watu elfu 45 wameripotiwa kuaga dunia katika janga hilo la kimaumbile.