Saudia yamwalika Rais Assad wa Syria katika kikao cha Riyadh cha viongozi wa Arab League
Apr 03, 2023 22:41 UTC
Shirika la habari Reuters limeripoti kuwa, Saudi Arabia inapanga kumualika Rais Bashar al-Assad wa Syria kuhudhuria mkutano ujao wa wakuu wa nchi za Kiarabu.
Mnamo mwaka 2012, Saudi Arabia ilivunja uhusiano wa kidiplomasia na Syria na kufunga ofisi yake ya kibalozi mjini Damascus.
Reuters imetangaza kuwa, baada ya zaidi ya muongo mmoja wa kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Syria, serikali ya Saudi Arabia inapanga kumwalika Rais Bashar al-Assad wa Syria ashiriki katika mkutano wa wakuu wa nchi za Kiarabu, utakaofanyika Mei 19 mjini Riyadh.
Shirika la habari la Reuters limeandika katika ripoti yake kuwa: Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan Al Saud atasafiri hadi Damascus katika wiki zijazo kufikisha mwaliko rasmi kwa Assad kushiriki katika mkutano huo wa Riyadh.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Machi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia ilithibitisha kuanza mazungumzo na Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria kwa ajili ya kuanzisha tena utoaji wa huduma za kibalozi.
Nchi nyingi za Kiarabu hivi karibuni zimetoa wito wa kurejeshwa Syria kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiarabu. Uwanachama wa Damascus katika jumuiya hiyo ulisimamishwa miaka 12 iliyopita kufuatia moto wa vita vya ndani nchini Syria uliowashwa na magenge ya kigaidi likiwemo la DAESH (ISIS) kwa uungaji mkono wa fedha na silaha wa madola ya Magharibi na baadhi ya tawala za Kiarabu za eneo la Asia Magharibi.../
Tags