Rais wa Syria afanya ziara ya kihistoria nchini Saudi Arabia + Video
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i97528-rais_wa_syria_afanya_ziara_ya_kihistoria_nchini_saudi_arabia_video
Rais Bashar al Assad wa Syria usiku wa kuamkia leo Ijumaa amewasili nchini Saudi Arabia kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ikiwa ni ziara ya kwanza ya kutembelea nchi hiyo tangu Syria ilipotumbukizwa kwenye mgogoro wa uvamizi wa magenge ya kigaidi.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
May 18, 2023 22:55 UTC

Rais Bashar al Assad wa Syria usiku wa kuamkia leo Ijumaa amewasili nchini Saudi Arabia kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ikiwa ni ziara ya kwanza ya kutembelea nchi hiyo tangu Syria ilipotumbukizwa kwenye mgogoro wa uvamizi wa magenge ya kigaidi.

Kwa mujibu wa gazeti la al Watan la Syria, ndege iliyombeba Rais Bashar al Assad ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Malik Abdulaziz mjini Jeddah Saudi Arabia, jana Alkhamisi usiku.

Rais Assad ameelekea nchini Saudia kwa mwaliko wa mfalme wa nchi hiyo, Salman bin Abdul Aziz na kwa ajili ya kushiriki kwenye kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa Arab League.

Rais Bashar al Assad wa Syria akishuka kutoka kwenye ndege mjini Jeddah, Saudi Arabia 

 

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Bashar al Assad kushiriki katika kikao cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu baada ya muongo mzima wa njama za kuitenga Syria.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Arab League walikuwa na kikao cha dharura hivi karibuni ambacho kilipasisha kurejeshwa Syria kwenye umoja huo.

Baada ya hapo vyombo vya habari duniani vilivyowanukuu maafisa wa kidiplomasia wa nchi za Kiarabu wakisema kuwa, Rais Bashar al Assad atashiriki katika kikao cha wakuu wa umoja huo cha nchini Saudi Arabia.

Kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa Arab League kinafanyika leo mjini Jeddah Saudi Arabia na kushiriki Rais wa Syria kwenye kikao hicho ni ushahidi wa kufeli njama zote za kieneo na kimataifa dhidi ya taifa hilo la Kiarbu.