Ansarullah ya Yemen yaionya Saudia isizike taka zake za nyuklia nchini Yemen
Harakati ya Ansarullah ya Yemen imeionya Saudi Arabia isithubutu kuzika taka zake za atomiki katika maeneo ya jangwani na baharini ya Yemen.
Mwezi Machi 2015, Saudi Arabia kwa uungaji mkono wa Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu hasa Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) ilianzisha uvamizi wa pande zote dhidi ya nchi maskini ya Kiarabu ya Yemen na kuiwekea vikwazo vya angani, ardhi na baharini nchi hiyo ya Waislamu.
Vikwazo hivyo havijaondolewa hadi hivi sasa na kwa mujibu wa shirika la habari la Sputnik, Wizara ya Uvuvi ya Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen imelaani jaribio la wavamizi wa Yemen wanaoongozwa na Saudia la kuigeuza Yemen kuwa pahala pa kuzikia uchafu wa sumu.
Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen imeonya kuhusu madhara makubwa ya taka hizo za sumu kwa wananchi wa Yemen. Wizara ya Uvuvi ya Yemen imesema, taka hizo ni hatari kubwa kwa mazingira na athari zake mbaya zitaendelea kuonekana hata katika miaka ya usoni.
Wizara hiyo imeongeza kuwa mionzi ya iliyogunduliwa katika Bahari ya Shamu na Bahari ya Arabia imesababisha vifo vya maelfu ya viumbe wa majini, uharibifu wa miamba ya matumbawe na mazingira ya baharini kwenye mwambao wa majimbo ya Aden, Abin, Al-Mahrah na Hadhramout.
Wizara ya Uvuvi ya Yemen pia imesema, Saudi Arabia imeigeuza Yemen kuwa uwanja wa majaribio kwa kila aina ya silaha zilizopigwa marufuku kimataifa, yakiwemo mabomu ya vishada, ambayo imepewa na washirika wake hasa Marekani, Israel na madola ya Magharibi kwa ajili ya kuwashambulia wananchi wa Yemen. ..