Aug 16, 2023 02:48 UTC
  • Taliban yaadhimisha mwaka wa pili wa kurudi madarakani Afghanistan huku ikiandamwa na lawama za UN

Kundi la Taliban la Afghanistan limeadhimisha mwaka wa pili wa kurejea madarakani kwa kuutangaza mnasaba huo kuwa siku rasmi ya mapumziko ikiwa ni kusherehekea kutekwa kwa mji mkuu Kabul na kuanzishwa kile kilichotajwa kuwa ni hali kamili ya usalama kote nchini chini ya uongozi wa "Mfumo wa Kiislamu".

Msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid ameeleza katika taarifa: "katika kumbukumbu ya mwaka wa pili wa kutekwa Kabul, tunapenda kulipongeza taifa la mujahidina la Afghanistan na kuwaomba wananchi wamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ushindi huu mkubwa".

Taarifa hiyo ya msemaji wa Taliban imeongezea kwa kusema: "hivi sasa, kwa vile kwa sehemu kubwa usalama umehakikishwa nchini, eneo lote la nchi linasimamiwa na liko chini ya uongozi mmoja, mfumo wa Kiislamu umewekwa na kila kitu kinafafanuliwa kutokana na mtazamo wa Sharia (Sheria ya Kiislamu)".

Usalama ulikuwa mkali mjini Kabul jana Jumanne katika maadhimisho hayo huku askari wakishadidisha hatua za upekuzi na ukaguzi.

Viongozi wa Taliban

Katika mji wa Herat magharibi mwa Afghanistan, umati mkubwa wa wafuasi wa Taliban waliandamana huku wakitoa nara na kaulimbiu za: "mauti kwa Ulaya, mauti kwa Magharibi, idumu Imarati ya Kiislamu ya Afghanistan, mauti kwa Marekani."

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, tangu Taliban irudi madarakani miaka miwili iliyopita, Afghanistan imepata amani na usalama kwa kiwango ambacho hakijashuhudiwa katika miongo kadhaa, licha ya ripoti za Umoja wa Mataifa kwamba kumekuwepo na makumi ya mashambulizi dhidi ya raia, ambayo baadhi ya watu wanasema, yamehusisha kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS).

Hayo yamejiri huku wataalamu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu wakikosoa ripoti za kila mara za uongozi wa Taliban zinazodai kuwa serikali ya kundi hilo inazifanyia marekebisho sera zake. Ripoti ya wataalamu hao imesisitiza kuwa licha ya kauli hizo, Taliban ingali inatekeleza mifumo ya ubaguzi, uenguaji na ukandamizaji wa wanawake na wasichana.

Katika ripoti yao hiyo waliyoitoa mjini Geneva, Uswisi, wataalamu hao wamesema, miaka miwili iliyopita Wataliban walitwaa madaraka Afghanistan na tangu wakati huo sera walizowawekea wananchi wa taifa hilo zimesababisha mwendelezo wa mfumo wa ufutaji haki kadhaa za kibinadamu, ikiwemo haki ya elimu, ajira, uhuru wa kujieleza na kukusanyika.../

 

Tags