Sep 21, 2023 03:49 UTC
  • Erdogan na Anwar Ibrahim walaani kuvunjiwa heshima Qur'ani katika nchi za Ulaya

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, na Waziri Mkuu wa Malaysia, Anwar Ibrahim, wamelaani vikali vitendo vya kuchomwa moto nakala za Qur'ani Tukufu katika nchi za Ulaya, na hotuba zinazochochea ouvu, chuki na mashambulizi dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Idara ya Mawasiliano ya Ofisi ya Rais wa Uturuki imesema katika taarifa yake jana, Jumatano kwamba Erdogan na Ibrahim wametoa taarifa ya pamoja kuhusiana na ongezeko la vitendo vya chuki, ubaguzi na unyanyasaji dhidi ya Waislamu na matukufu yao.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na viongozi hao wawili imesema: "Tunalaani kwa nguvu zote matukio ya kuchomwa moto nakala za Qur'ani Tukufu yaliyotukia hivi karibuni katika baadhi ya nchi za Ulaya chini ya kivuli cha uhuru wa kujieleza, pamoja na matamshi yanayohimiza unyanyasaji, kauli za chuki na mashambulizi dhidi ya Uislamu na Waislamu.”

Erdogan (kulia) na Anwar Ibrahim

Taarifa hiyo imekaribisha hatua ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Machi 2022 ya kupitisha Azimio Namba 254/76 la kuitangaza Machi 15 kila mwaka kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Chuki dhidi ya Uislamu.

Vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika baadhi ya nchi za Ulaya zinazodai kutetea haki za binadamu na uhuru katika miezi ya hivi karibuni, hususan huko Sweden na Denmark, vimezusha hasira kubwa za Waislamu kote dunia.

Mgogoro wa kuchoma nakala za Qur’ani Tukufu umezusha maswali mengi kuhusu mipaka ya uhuru wa kujieleza na haki ya kuumiza hisia za kidini.

Tags