Sep 24, 2023 07:48 UTC
  • Papa Francis: Nchi za Magharibi zinatumia vita vya Ukraine kujinufaisha

Kiongozi wa Wakatoliki duniani amezitaka baadhi ya nchi "ziache kucheza" na misaada ya silaha kwa serikali ya Ukraine.

Papa Francis, ambaye amemtuma Kadinali wa Italia, Matteo Zoppi kwenda Kiev, Moscow, Washington na Beijing kujadili hali ya Ukraine na kuanzisha mchakato wa amani, alisema jana Jumamosi akirejea kutoka safari ya mji wa bandari wa Marseille nchini Ufaransa, kwamba anahisi kukata tamaa kuhusu juhudi za kurejesha amani nchini Ukraine.

Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Papa Francis amezungumzia jinsi nchi za Magharibi zinavyofaidika na vita vya Ukraine na kusema: Kwa maoni yangu, maslahi ya vita vya Ukraine hayahusiane tu na tatizo la Ukraine na Russia, bali pia yanahusiana na mauzo na biashara ya silaha.

Msimamo mpya wa Papa wa kanisa Katoliki dhidi ya kupeleka silaha Ukraine unakuja baada ya kusema mwaka jana kuwa, ni halali kimaadili kutoa silaha kwa Ukraine ili kujilinda dhidi ya Russia.

Tangu kuanza kwa vita kati ya Russia na Ukraine mnamo Februari 2022, Marekani imekuwa ikiongoza himaya na misaada ya nchi za Magharibi kwa Kiev, na Bunge la Marekani limeidhinisha msaada wa zaidi ya dola bilioni 100 kwa Ukraine, zikiwemo dola bilioni 43 zilizotumika kununua silaha.