Sep 24, 2023 10:53 UTC
  • Russia: Fatwa ya Ayatullah Khamenei inatosha kuthibitisha kuwa Iran haina ratiba ya kumiliki silaha za nyuklia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, fatwa ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei inatosha kuthibitisha kuwa Iran haina ratiba zozote za kumiliki silaha za atomiki.

Hata Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA nao umesema mara chungu nzima kwenye ripoti zake kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina ratiba zozote za kumiliki silaha za atomiki na kwamba mradi wake wa nyuklia ni wa amani kikamilifu. 

Kwa upande wake, Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikisisitiza waziwazi kwamba, kutokana na kuwa kwake nchi iliyotia saini Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Atomiki (NPT), ina haki ya kufaidika na teknolojia ya nyuklia kwa matumizi ya amani.

Sergey Lavrov akizungumza na waandishi wa habari mjini New York Marekani

 

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia alisema jana Jumamosi mbele ya waandishi wa habari pambizoni mwa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kwamba, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran ametoa fatwa ya kidini ya kuharamisha matumizi ya bomu la atomiki. Amesema, mara chungu nzima Iran imekuwa ikisema kuwa, haina nia kabisa ya kumiliki silaha hizo (kutokana na kuwa ni za kuua watu kwa umati).

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema, kufikia hatua Kiongozi Mkuu wa kidini wa Iran kutoa fatwa ya kuharamisha matumizi ya silaha za nyuklia, inatosha kwetu kuamini kuwa Iran haitomiliki bomu la nyuklia na hakuna sababu yoyote kwa majirani wa Iran kuwa na wasiwasi kuhusu suala hilo. Amesema, hakuna nchi yoyote inayopenda kuona kunachipuka nchi nyingine za silaha za nyuklia duniani.