Oct 16, 2023 12:13 UTC
  • Kukaririwa mauaji ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watoto huko Marekani kwa kuuawa kinyama mtoto wa Kipalestina

Polisi ya Chicago imetangaza kuwa mkazi mmoja wa mji huo amemuua mvulana wa Kipalestina wa miaka 6 kwa kisu na kumjeruhi vibaya mama yake.

Polisi imelaani kitendo hicho cha mabavu na kukitaja kuwa kipumbavu na cha woga. Baraza la Mahusiano ya Kiislamu la Marekani limetangaza kwamba mtenda jinai huyo alikuwa akipiga nara za chuki dhidi ya Palestina na Uislamu wakati wa kitenda hicho. Baraza hilo limetaka kukomeshwa chuki dhidi ya Uislamu na Palestina miongoni mwa wanasiasa wa Marekani na vyombo vya habari vya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa polisi, kijana huyo alidungwa kisu mara 26 na mmiliki wa nyumba hiyo mwenye umri wa miaka 71 huko Plainfield na kufariki dunia akiwa hospitalini. Maafisa wa Polisi wa Chicago wamesema kuwa Mama yake mwenye umri wa miaka 32 pia amepata majeraha kadhaa ya visu na anaendelea na matibabu hospitalini. Katili huyo kwa jina Joseph Czuba ameshtakiwa kwa mauaji ya daraja la kwanza, jaribio la kuua na kujeruhi.

Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Will huko Chicago imesema katika taarifa yake kwamba Wapelelezi wameweza kubaini kwamba wahasiriwa wote wa shambulio hilo la kikatili walilengwa kwa sababu walikuwa ni Waislamu na kutokana na mzozo wa Mashariki ya Kati kati ya Hamas na Israeli. Kitendo hicho ni  cha kinyama kwa kadiri kwamba Ikulu ya White House pia imelazimika kukilaani. Rais Joe Biden wa Marekani ameandika kwenye X   alipopata habari kuhusu mauaji ya kikatili ya mtoto huyo na kujeruhiwa mama yake huko Illinois kuwa kitendo hicho cha kuchukia familia ya Kiislamu  na ya Palestina hakina nafasi nchini Marekani. Amesema Wamarekani wanapaswa kuungana na kukataa chuki zilizo dhidi ya Uislamu na ubaguzi wa aina yoyote ile. Kwa kuzingatia msimamo huo wa Biden, swali linajitokeza hapa kuwa je, ni kwa nini amenyamazia kimya mauaji ya watoto yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko katika Ukanda wa Gaza, bali anayaunga mkono kwa njia isiyo ya moja kwa moja?

Mjomba wa mtoto wa Kipalestina akiwa katika Idara ya Baraza la Mahusiano ya Kiislamu

Kitendo cha kijinai cha Mmarekani huyo mwenye msimamo mkali anayeunga mkono Israel katika mauaji ya kinyama na kikatili dhidi ya mtoto wa Kipalestina kinaendeleza siasa za kila siku za  utawala wa Israel za kuwauwa watoto wa Palestina. Baada ya kuanza operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa na wakati wa mashambulizi ya kutisha ya anga ya jeshi la Utawala wa Kizayuni katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Ghaza, Wapalestina 2670 wameuawa shahidi ambapo zaidi ya 700 kati yao ni watoto.

Mtandao wa Quds wa Palestina umetangaza kuwa idadi ya watoto wa Kipalestina waliouawa shahidi kupitia hujuma ya mabomu ya Israel ndani ya wiki moja ni zaidi ya idadi ya watoto wa Ukraine waliouawa katika kipindi cha miezi 20 iliyopita. Msemaji wa UNICEF amesisitiza kuwa "hakuna tena mahali salama kwa watoto huko Gaza, wala maji, chakula na dawa havipatikani.

Wakati huo huo jinai ya raia huyo wa Marekani inaonyesha kuenea kwa misimamo mikali na chuki za ubaguzi nchini Marekani.

Eneo la tukio

Kuhusiana na hilo, Christopher Ray, Mkuu wa FBI ameonya juu ya kuongezeka  misimamo mikali ya kikatili kufuatia mzozo kati ya Hamas na Israel na kusema: hakuna shaka kuwa vitisho hivyo vitaongezeka nchini humo.

Kwa kuzingatia mwenendo wa vitisho unaoongezeka dhidi ya Waislamu nchini Marekani, Baraza la Mahusiano ya Kiislamu la Marekani limetoa wito wa kukomeshwa chuki dhidi ya Uislamu na Palestina miongoni mwa wanasiasa na vyombo vya habari vya Marekani. Chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini humo imeongezeka tokea kipindi cha utawala wa urais wa Donald Trump, ambaye alikuwa na chuki ya moja kwa moja dhidi ya Uislamu na Waislamu. Hivi sasa nchini Marekani vitendo vya ubaguzi na unyanyasaji wa kimwili na wa maneno dhidi ya Waislamu vimeongezeka kutokana na kuongezeka kwa kiasi kikubwa makundi ya mrengo wa kulia pamoja na propaganda za vyombo vya habari dhidi ya Waislamu hususan baada ya matukio ya hivi karibuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Mwenendo huo unajumuisha mashambulizi ya kikatili dhidi ya Waislamu, hasa wale wanaofanana na watu kutoka nchi za Kiislamu za Asia Magharibi. Kuchomwa moto maeneo ya ibada ya Waislamu, mashambulizi ya maneno na vitisho dhidi ya Waislamu na kubaguliwa Waislamu katika taasisi mbalimbali za kielimu na kikazi na kuongezeka chuki dhidi ya Waislamu katika vyombo vya habari vya Marekani ni baadhi ya vitendo hivyo vya chuki. Jinai ya hivi karibuni dhidi ya mama na mtoto wa Kiislamu huko Chicago pia imetokea kutokana na kuongezeka anga ya chuki dhidi ya Waislamu nchini Marekani katika kivuli cha vita kati ya Hamas na utawala wa Kizayuni.

 

 

Tags