Kuendelea mashambulizi ya kigaidi huko Herat Afghanistan na maswali yasiyo na majibu
Katika hali ambayo hazijapita siku nyingi tangu viongozi wa kieneo wa kundi la Taliban huko Herat na pia wakazi wa mji mkuu Kabul watoe ahadi ya kuwadhaminia wananchi usalama wao khususan Waislamu wa Kishia na maulamaa wao, mji wa Herat kwa mara nyingine tena umeshuhudia mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Waislamu wa Kishia yaliyosababisha kuuliwa Maulamaa wao wawili.
Katika wiki za karibuni mashambulizi dhidi ya Waislamu wa Kishia khususan maulamaa wa kidini katika mji wa Herat yameongezeka, na kile ambacho zaidi kinawatia wasiwasi wananchi wa Afghanistan ni mauaji makubwa yaliyoratibiwa vilivyo na kwa malengo maalumu, ya kuwauwa maulamaa wa kidini; kiasi kwamba tarehe 23 mwezi ulioisha wa Novemba watu wasiojulikana wenye silaha walifanya shambulio la kigaidi katikati ya mji wa Herat na kuwauwa maulamaa wawili wa Kishia.
Hata kama viongozi wa kieneo wa Taliban wameahidi kuwa watazuia kurudiwa mashambulizi kama hayo lakini magaidi kwa kurudia kufanya jinai hiyo huko Herat wamejaribu kuonyesha kuwa kundi la Taliban linalotawala Afghanistan haliwezi kuwadhaminia usalama watu wa nchi hiyo na bado magaidi wanaweza kufanya mauaji na kusababisha ukosefu wa usalama na kuibua hofu nchini humo. Najma Iqbal mchambuzi wa masuala ya kiusalama na kiistratejia anazungumzia suala hili kwa kusema:" Magaidi wanaendeleza mauaji yaliyoratibiwa kwa malengo mawili makuu huko Afghanistan. Mosi ni kwa ajili ya kujaribu kuutahini uwezo na nguvu za Taliban katika kudhamini usalama wa wananchi wa Afghanistan na pili, magaidi wanafanya hivyo ili kuisukuma Afghanistan katika vita vya ndani vya kimadhehebu. Hata kama habari na taarifa zinazotangazwa zinajaribu kuonesha kuwa, magaidi ni watu wasiojulikana lakini ni vigumu kukubali kwamba Taliban haiwafahamu watu hao na au kuwa kundi hilo halina uwezo wa kuwatambua magaidi hao.
Ikiwa ripoti za duru za ndani huko Herat kwamba watu wanane walipigwa risasi wakiwa njiani kuelekea katika kitongoji cha Shuhada na huko Sabz katika mji wa Herat ni za kweli basi rekodi ya utendaji wa maafisa wa usalama wa Taliban huko Herat inapasa kuwa na alama isiyoridhisha. Watu watano wameuliwa shahidi na wengine watatu wamejeruhiwa vibaya katika shambulizi hilo la kigaidi. Imeelezwa kuwa risasi zilimiminwa kutoka nani ya gari moja kushambulia bajaji iliyokuwa na watu wawili waliotajwa kuwa ni maulamaa wa Kishia waliokuwa pamoja na familia zao.
Katika miongo kadhaa iliyopita ambapo Afghanistan ilikumbwa na matatizo ya ndani na kukaliwa kwa mabavu na nchi ajinabi nchi hiyo haikuwahi kuelekea upande wa vita au mapigano ya kidini na siku zote migogoro ya nchi hiyo chimbuko lake lilikuwa ni masuala ya kikabila. Lakini tokea Taliban ishike tena hatamu za uongozi huko Afghanistan katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili iliyopita, mashambulizi makubwa ya kigaidi yamekuwa yakifanywa katika maeneo ya kidini na kuwalenga maulamaa; jambo linalodhihirisha kuwepo harakati za mirengo iliyoratibiwa vilivyo ya kigaidi ambayo chimbuko lake ni nje ya Afghanistan. Sayyid Issa Mazari anasema kuhusiana na hili kwamba: Wananchi wa Afghanistan imma ni Washia au ni Wasuni na siku zote wanaishi kwa amani na maelewano na kamwe hawatoi mwanya kwa maadui wa Afghanistan kuvuruga maelewano yao. Hata hivyo hujuma za magaidi katika miaka ya hivi karibuni ikiwa ni pamoja na kushambulia maeneo ya kidini na maulamaa wa kidini zinaonyesha kuingia mrengo wa kigaidi unaopenda machafuko huko Afghanistan ambao utatishia sana usalama wa nchi hiyo iwapo Taliban itashindwa kuusaka haraka na kuuangamiza."
Kiujumla ni kwamba, wananchi wa Afghanistan wanataraji kuwa serikali ya Taliban itatekeleza ahadi yake kwa kuwabaini na kuwatia mbaroni magaidi hao na kurejesha usalama na amani kwa jamii ya Afghanistan. Kinyume na hivi, kundi hilo lielewe kuwa, zipo pande zinazofanya kazi ya kuchochea vita vya kidini huko Afghanistan, na ikiwa wigo wake utapanuka, itakuwa ngumu mno kwa Taliban kudhibiti hali hiyo ya mambo.