Dec 07, 2023 11:58 UTC
  • Barua isiyo ya kawaida ya Guterres kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Gaza

Katika hatua isiyo ya kawaida, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametumia mamlaka aliyopewa kisheria kupitia kifungu cha 99 cha Hati ya Umoja wa Mataifa kulishinikiza Baraza la Usalama la umoja huo lianzishe haraka usitishaji vita huko katika Ukanda wa Gaza.

Kifungu hicho, ambacho kimetumika mara 9 pekee katika historia nzima ya Umoja wa Mataifa, kinamruhusu katibu mkuu wa umoja huo kuwaalika wajumbe wa Baraza la Usalama kwenye mkutano wa dharura na kuwataka wachukue hatua za dharura kwa ajili ya  kukabiliana na kile anahisi kinahatarisha "usalama na amani ya dunia."

Jumatano jioni, Antonio Guterres alituma barua kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya kusikitisha ya Ukanda wa Gaza. Amesambaza barua hiyo kwa kuzingatia Kifungu cha 99 cha Hati ya Umoja wa Mataifa, ambacho kinahusu kuhatarishwa usalama wa dunia. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya katika barua hiyo kwa kusema: "Hali ya Gaza inatishia amani na usalama wa kimataifa, na jamii ya kimataifa inapaswa kutumia ushawishi wake kumaliza mgogoro huu." Guterres amewataka wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa mashinikizo ya kuzuia mgogoro wa kibinadamu na kutoa wito wa kuanzishwa usitishaji vita wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Barua ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Baraza la Usalama inaonyesha kuharibika kusiko kwa kawaida kwa hali ya Ukanda wa Gaza na kuzuka maafa ya kibinadamu katika eneo hilo la Palestina, kutokana na kuendelea mashambulizi ya kikatili ya anga na ya nchi kavu yanayofanywa na utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya raia wasio na hatia. Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya Wapalestina 16,000 katika Ukanda wa Gaza, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake, wameuawa shahidi na zaidi ya 34,000 wamejeruhiwa.

Jinai za Wazayuni Gaza

Hayo yanajiri katika hali ambayo imekuwa vigumu kuwahudumiwa majeruhi na kuzika miili ya mashahidi wa mauji hayo ya kimbari kutokana na mashambulizi ya kinyama ya mabomu yanayofanywa na utawala huo wa Kizayuni katika majengo ya hospitali. Pamoja na hayo lakini watawala wa Tel Aviv wanasisitiza juu ya kuendelea kufanya mashambulizi hayo ya kikatili. Baada ya kumalizika usitishaji vita wa siku 7, utawala wa Kizayuni umeshadidisha mashambulizi yake dhidi ya raia wa ukunda huo. Mashambulizi hayo ambayo ni makali sana na yasiyo na huruma, yamesababisha vifo vya idadi kubwa ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na kupelekea maelfu ya wengine kukimbia makaazi yao. Yoav Gallant, Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni amesema katika mahojiano: "Tunatabiri kwamba vita (huko Gaza) vitaendelea kwa kasi yake ya hivi sasa kwa angalau miezi mingine miwili. Baada ya hapo, operesheni ya "kusafisha" itafanyika ili kuondoa makundi ya Hamas."

Matamshi hayo yanaonyesha kuwa, licha ya mashinikizo ya kimataifa ya kutaka kusitishwa mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza, lakini bado viongozi waandamizi wa utawala huo wanasisitiza kuendeleza mashambulizi hayo ya kinyama na hilo linatokana na uungaji mkono mkubwa wa kisiasa na kijeshi wanaoupata kutoka kwa Marekani. Hii ndio maana hata yale maeneo yaliyotangazwa na utawala huo wenyewe kuwa ni salama pia yamekuwa yakishambuliwa kwa mabomu bila huruma. John Kirby, Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani huku akipinga matumizi ya maneno 'maangamizi ya kizazi' yaliyotumiwa na waungaji mkono wa haki za wananchi wa Palestina kuhusiana na mauaji ya halaiki yanayofanywa na utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi raia wa Gaza, amedai kuwa maneno hayo yanapaswa kutumika kuhusu Hamas.

Watu wa Gaza hivi sasa hawana maeneo salama, si kaskazini, katikati, wala hata kusini mwa Gaza kutokana na mashambulizi makali ya mabomu na makombora ya jeshi la Kizayuni katika kila nukta ya ukanda huo, ambapo ndege za utawala huo zinashambulia kwa mabomu shule na maeneo mengine yanayosimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa UNRWA. Ayman al-Safadi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan, alisema siku ya Jumatano kwamba: "Vitendo ambavyo Israel inavifanya ni mauaji ya kimbari dhidi ya taifa la Palestina." Hatuwezi kukubali kimya cha jamii ya kimataifa, ambayo inafunika mashambulizi ya kinyama ya Israel."

Suala muhimu linalopaswa kuzingatiwa hapa ni kwamba licha ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutochukua hatua sambamba na ushirikiano wa serikali za Magharibi na Tel Aviv katika maangamizi ya umati ya watu wa Gaza, lakini katika ngazi ya kimataifa hususan katika nchi za Magharibi, maandamano makubwa yamekuwa yakifanywa na wananchi wa nchi hizo kwa miezi miwili iliyopita, kwa lengo la kulaani vitendo vya jinai vya utawala wa Kizayuni na kutaka kusitishwa mara moja mashambulizi hayo ya kikatili dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Gaza.

Ukatili wa Wazayuni dhidi ya raia wa Palestina

Aidha, sasa makundi na mashirika yasiyo ya kiserikali yanatakai kusitishwa mara moja hujuma ya Wazayuni dhidi ya raia huko Gaza. Katika hatua ya karibuni kuhusiana na suala hilo, wanafunzi 40 wanaojifunza masuala mbalimbali katika Ikulu ya White House wamemwandikia barua ya wazi Rais Joe Biden wa Marekani, wakimkosoa kwa kupuuza matakwa ya watu wa Marekani ya kuanzishwa usitishaji vita huko Gaza na kutaka suala hilo lishughulikiwe haraka iwezekanavyo. Wakati huo huo, uungaji mkono wa Biden kwa mashambulio ya kikatili ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza umeibua lawama kali kutoka kwa mrengo endelevu wa chama cha Democrat. Rashida Tlaib, mjumbe wa chama hicho katika Baraza la Wawakilishi la Marekani, amesema: Joe Biden anaunga mkono "mauaji ya halaiki" dhidi ya Wapalestina katika vita vya Gaza, na Wamarekani hawatasahau suala hili katika uchaguzi wa 2024.

Tags