Dec 08, 2023 03:18 UTC
  • Uhispania yamtetea Katibu Mkuu wa UN, yasema hali ya Gaza ni janga lisilovumilika

Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez, ametangaza "uungaji mkono wake kamili" kwa barua ambayo haijawahi kushuhudiwa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akitaka kusitishwa vita Ukanda wa Gaza kwa sababu za kibinadamu.

Pedro Sanchez amesema yanayojiri katika eneo la Ukanda wa Gaza ni majanga ambayo hayawezi kustahamilika. 

Waziri Mkuu wa Uhispania ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba, "Janga la kibinadamu huko Gaza haliwezi kuvumilika. Ninaelezea uungaji mkono wangu kamili kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, katika kutekeleza Kifungu cha 99 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa."

Amesisitiza kuwa: Kwa kuzingatia hatari ya kuporomoka hali ya kibinadamu huko Gaza, Baraza la Usalama linapaswa kuchukua hatua mara moja.

Uungaji mkono wa Waziri Mkuu wa Uhispania kwa Katibu Mkuu wa UN unakuja siku moja baada ya Israel kuanzisha mashambulizi makali dhidi ya Antonio Guterres, na kusisitiza kwamba anapaswa kujiuzulu baada ya wito wake wa kusitisha vita na mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Eli Cohen amedai katika hujuma kali dhidi ya Katibu Mkuu wa UN kwamba: "Muhula wa Guterres ni tishio kwa amani duniani!"

Cohen amedai kwamba ombi la Guterres la kutekelezwa Kifungu cha 99 cha Hati ya UN na wito wa kusitishwa kwa mapigano huko Gaza ni "uungaji mkono kwa kundi la kigaidi la Hamas."

Hujuma kali ya utawala ghasibu wa Israel inafuatia hatua ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ya kutumia ibara ya 99 ya Hati ya Umoja wa Mataifa, ambayo ni nadra sana kutumiwa na Katibu Mkuu wa umoja huo, akilitolea wito mzito Baraza la Usalama wa "kushinikiza kuepusha janga la kibinadamu" katika Ukanda wa Gaza na kuungana katika kutoa wito wa kusitishwa kikamilifu mapigano na mashambulizi ya Israel Ukanda wa Gaza.

Ibara hiyo ya 99 iliyoko katika Sura ya 15 ya Hati ya Umoja wa Mataifa inasema, mkuu huyo wa UN "anaweza kulijulisha Baraza la Usalama jambo lolote ambalo kwa maoni yake, linaweza kutishia amani na usalama wa kimataifa."