Feb 24, 2024 02:16 UTC
  • Mshirika wa Putin ataka al Houthi wapewe silaha za kushambulia meli za Marekani na Uingereza

Afisa maarufu wa propaganda wa Lkulu ya Rais wa Russia, Kremlin, amesema kwamba Moscow inapaswa kuwapa wapiganaji wa harakati ya Ansarullah wa Yemeni silaha za kisasa kwa ajili ya kutumiwa katika mashambulizi dhidi ya meli za Marekani na Uingereza kwenye Bahari Nyekundu.

Vladimir Solovyov, mtu mashuhuri katika vyombo vya habari vinavyoungwa mkono na Kremlin na mshirika mkubwa wa Rais Vladimir Putin, ametoa pendekezo hili katika kipindi cha matangazo yake kwenye kituo cha Rossiya-1.

Jarida la Newsweek limeripoti kwamba, matamshi hayo ya  Solovyov yametolewa wakati mapigano yakiendelea katika Bahari Nyekundu kati ya wapiganaji wa harakati ya Ansarullah ya Yemen na majeshi ya Marekani na Uingereza.

Vladimir Solovyov amesema, Moscow inapaswa kuwapa Wahouthi wa Yemen silaha ili kulipiza kisasi kwa nchi za Magharibi ambazo zinaendelea kuisaidia Ukraine katika vita vyake dhidi ya vikosi vya jeshi ta Russia.

Solovyov ametoa wito wa kulipatia kundi hilo silaha za kisasa ili kuanzisha mashambulizi dhidi ya ngome na maeneo ya Marekani na Uingereza, akisema: "Huu ndio wakati mwafaka."

Amesema: "Wapiganaji wa Kihouthi watapata kila kitu. Watakuwa na boti na silaha zenye nguvu, na watapata kila kitu."

Jarida la Newsweek limeeleza kuwa, mwezi mwezi Oktoba mwaka jana Solovyov aligonga vichwa vya habari alipoonya kuhusu vita vipya vya dunia ambavyo vitazifanya nchi za Magharibi kusimama dhidi ya Waislamu duniani kote.

Vikosi vya jeshi la Yemen vimeahidi kuwa vitaendelea kushambulia meli za Israel au zile zinazoelekea kwenye bandari zake huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu hadi utawala huo wa Kizayuni utakaposimamisha mashambulio yake dhidi ya Gaza. 

Ansarullah wanashambulia meli zote zinazopeleka bidhaa Israel

Wakati huohuo, vikosi vya jeshi la Yemen vimesisitiza na kutamka bayana kuwa, meli nyingine zote ziko huru na zitakuwa na usalama kamili wa kufanya safari zao za baharini katika Ghuba ya Aden na Bahari Nyekundu.