Feb 26, 2024 07:01 UTC
  • Mwanajeshi wa Marekani ajichoma moto nje ya ubalozi wa Israel mjini Washington

Mwanamume mmoja amelazwa hospitalini akiwa katika hali mbaya baada ya kujichoma moto nje ya Ubalozi wa utawala haramu wa Israel huko Washington, DC siku ya Jumapili kulalamikia mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala huo dhidi ya Wapalestina wa Gaza.

Vito Maggiolo, msemaji wa Idara ya Zimamoto Washington DC, amewaambia waandishi wa habari kwamba mtu huyo amelazwa hospitalini na "majeraha mabaya ya kutishia maisha."

Picha za tukio hilo zinaonyesha mtu huyo alikuwa amevalia sare ya kijeshi na alijitambulisha kama "afisa wa Jeshi la Anga la Marekani."

Walioshuhudia wanasema askari huyo alisikika akisema "Sitashiriki tena katika mauaji ya kimbari" huku akipaza sauti na kusema "Palestine Huru."

CNN, ambayo pia ilipitia video hiyo, ilisema kuwa mtu huyo alijitambulisha kama Aaron Bushnell. Msemaji wa Jeshi la Anga la Marekani Rose Riley baadaye aliithibitishia CNN kwamba "afisa ambaye hivi sasa yuko katika Jeshi la Anga ndiye aliyejiteketeza katika tukio hilo."

Maandamano mengi ya kuunga mkono Palestina yamekuwa yakifanyika nje ya balozi za utawala haramu wa Israel katika maeneo mbali mbali duniani baada ya utawala huo kuanzisha mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza mwezi Oktoba 2023. Waandamanaji hao wamekuwa wakitaka kusitishwa vita vya Israel dhidi Gaza kutokana na idadi kubwa ya vifo vya raia. Mapema mwezi wa Disemba, mwanamume mmoja alijichoma moto mbele ya ubalozi mdogo wa utawala wa Israel huko Atlanta, Georgia.

Kwa ujumla maandamano ya kuupinga utawala wa Kizayuni wa Israel na kuunga mkono Wapalestina wanaodhulumiwa yamekuwa yakifanyika kote duniani karibu kila siku. Maandamano hayo pia yameshadidi katika nchi za Magharibi hasa Marekani, ambayo inashirikiana na utawala haramu wa Israel katika mauji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.