Feb 28, 2024 02:49 UTC
  • Russia: Vita havitaepukika Ulaya ikiwa NATO itapeleka wanajeshi Ukraine

Russia imezionya nchi wanachama wa muungano wa kijeshi wa NATO barani Ulaya kuhusu vita vinavyoweza kutokea iwapo nchi za muungano huo zitapeleka wanajeshi Ukraine.

Tangaza hilo la Russia limekuja  siku moja baada ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kuzungumzia waziwazi uwezekano wa kutuma wanajeshi wa Ulaya nchini Ukraine.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema Jumanne kwamba Ulaya na Marekani zinapaswa "kutathmini" msaada wao kwa Ukraine.

"Katika kadhia hii, tunahitaji kuzungumza sio juu ya uwezekano, lakini juu ya kutoepukika kwa mzozo," Peskov alinukuliwa akisema.

"Nchi hizi lazima pia zitathmini na kufahamu hili, zikijiuliza kama hii ni kwa maslahi yao, pamoja na maslahi ya raia wa nchi zao," aliwaambia waandishi wa habari.

Siku ya Jumatatu, rais wa Ufaransa alisema kuwa uwezekano wa kupeleka wanajeshi Ukraine hauwezi kufutwa, licha ya kukosekana kwa "makubaliano" juu ya suala hilo.

"Hakuna makubaliano katika hatua hii... kutuma wanajeshi wan chi kavu," Macron alisema.

Aliongeza kuwa: "Tutafanya kila tuwezalo ili Urusi isishinde.”

Russia imeonya mara kwa mara juu ya athari za kuendelea kwa msaada wa kijeshi wa Magharibi kwa Ukraine. Kambi ya Magharibi imepuuza onyo hilo. Kiev imefurahia mtiririko wa mara kwa mara wa msaada wa kijeshi wenye thamani ya mabilioni ya dola tangu kuanza kwa mzozo Februari 2022.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov

Mnamo mwaka wa 2023, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov alisema Marekani, Uingereza na wengine wengi "wako vitani  dhidi ya Russia na wanashiriki katika uhasama dhidi ya nchi hiyo kwa kuisaidia Ukraine.

Wakati huo huo, nchi kadhaa za Ulaya zimetangaza kutotaka kupeleka wanajeshi Ukraine.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz Jumanne alifutilia mbali mapendekezo kwamba nchi za Ulaya na wanachama wa NATO watatuma wanajeshi wa nchi kavu  nchini Ukraine.

Msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak alisema Uingereza haina mpango wa kupeleka wanajeshi Ukraine pia.

Hungary na Slovakia pia hazikusudii kufanya uwekaji huo wa wanajeshi.

Na Waziri Mkuu wa Poland, Donald Tusk, mmoja wa wafuasi sugu wa Ukraine, pia amekuwa wazi juu ya kutoshiriki askari wa NATO katika medani ya moja kwa moja vitani nchini Ukraine.