Feb 29, 2024 02:30 UTC
  • Kukiri Borrell juu ya mwisho wa udhibiti wa Magharibi duniani kutokana na vita vya Ukraine na Gaza

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amekiri kuwa udhibiti wa nchi za Magharibi duniani umeyoyoma na kumalizika baada ya kuanza operesheni maalumu ya kijeshi ya Russia huko Ukraine na vita Israel huko Ukanda wa Gaza

Josep Borrell anaamini kwamba, ikiwa mvutano wa sasa wa siasa za kijiografia (geopolitical) wa kimataifa utaendelea kwa upande wa "Magharibi dhidi ya wengine", hatari kwa Ulaya itakuwa kubwa zaidi katika siku zijazo. Borrell amekiri kwamba: "Enzi ya utawala na udhibiti wa Magharibi imekwisha. Ingawa hili linaeleweka kinadharia, lakini sisi bado hatujaielewa na kulikubali". Borrell anasema, operesheni maalumu ya kijeshi nchini Ukraine na vita vya Gaza vimeongeza kwa kiasi kikubwa hatari ya makabiliano kati ya Magharibi na Kusini. 

Kukiri kwa Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya kwamba ushawishi na hata udhibiti wa Wamagharibi duniani katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi umemalizika, hasa baada ya kutokea vita viwili vikubwa katika maeneo mawili nyeti ya dunia yaani vita vya Ukraine barani Ulaya na vita vya Gaza huko Asia Magharibi, kunathibitisha na kutia nguvu mtazamo wa wakosoaji wa nchi za Magharibi katika uwanja huu, yaani kuporomoka udhibiti wa Magharibi hususan Marekani.

Joe Biden

Ingawa Borrell ametumia neno "Magharibi na Kusini" kugawanya ulimwengu kati ya nchi za Magharibi na zisizo za Magharibi, jambo ambalo lenyewe ni ishara ya kujiona bora na juu zaidi watu wa Ulaya kuliko mataifa mengine, lakini ukweli ni kwamba, kwa kuzingatia matukio ya kimataifa katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijeshi, haswa kuibuka kwa nguvu mpya za kimataifa kama vile Uchina, Russia, India, Brazil na Afrika Kusini, ambazo zimeunganishwa katika makundi kama BRICS na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, na vilevile kuimarika fikra zisizo za Kimagharibi zinazosisitiza haja ya kutazazwa upya siasa na uchumi wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na katika Baraza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, inaonekana kuna changamoto kubwa dhidi ya kuendelea kuwepo udhibiti wa nchi za Magharibi duniani.

Hatua ya kwanza kabisa katika muktadha huu ni vita vya Ukraine ambavyo ni matokeo ya sera za kichokozi za nchi za Magharibi katika mfumo wa siasa za shirika la kijeshi la nchi za Magharibi, (NATO) za kujipanua upande wa Mashariki, juhudi za kuzipa uanachama nchi jirani na Russia, haswa Ukraine, katika jumuiya hiyo ya kijeshi na kupuuza maonyo ya Moscow katika uwanja huo. Russia imekuwa ikisema mara kwa mara kwamba, kutimia kwa jambo hili kuna maana ya kuhatarisha usalama wa taifa wa nchi hiyo. 

Sambamba na kuanza vita nchini Ukraine mnamo Februari 2022, Ulaya ikishirikiaina na Marekani, ilianza vita vya wakala dhidi ya Russia kwa kutuma silaha za makumi ya mabilioni ya dola na maelfu ya mamluki nchini Ukraine. Sasa, mwanzoni mwa mwaka wa tatu wa vita vya Ukraine, Russia imetoa pigo muhimu kwa Ukraine kwa kunyakua na kutwaa maeneo mengi ya majimbo 4 ya nchi hiyo, na pia kuuteka mji wa kimkakati wa Avdiivka, na kuitumbukiza serikali yenye mielekeo ya Kimagharibi ya Kiev katika hali mbaya na ngumu. Tunaweza kusema kuwa, vita vya Ukraine ni mpambano wa kupimana nguuvu na misuli kati ya Russia na NATO ikiongozwa na Marekani; na Wamagharibi wameshindwa katika makabiliano haya licha ya uwekezaji wao mkubwa. Kwa hivyo, vita vya Ukraine, kama anavyokiri Borrell, vinapaswa kutambuliwa kama kielelezo cha kushindwa na kuyoyoma udhibiti wa nchi za Magharibi.

Kwa upande mwingine, vita vya Gaza, vilivyoanza baada ya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa tarehe 7 Oktoba 2023, kwa mashambulizi makubwa ya anga na nchi kavu ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza, na hadi sasa vimesababisha uharibifu mkubwa na mauaji ya halaiki ya wakazi wa eneo, pia vimekuwa uwanja mwingine maonyesho ya kuporomoka ushawishi na taathira ya Magharibi katika masuala ya wa kikanda na kimataifa.

Japokuwa hapo awali, viongozi wa nchi za Magharibi kama Ujerumani, Uingereza na Ufaransa wakishirikiaina na Rais Joe Biden wa Marekani walikuwa wakipinga usitishaji vita na kutoa wito wa kuangamizwa kikamilifu makundi ya mapambano ya ukombozi ya Palestina hususan Hamas, lakini sasa maafisa hao wa Magharibi, akiwemo Josep Brrell, wanatoa wito wa kusitishwa vita hivyo vilivyoingia katika mwezi wa tano kutokana na Israel kushindwa kufikia malengo yake huko Gaza, kama vile kuangamizia harakati ya Hamas au kuwafukuza wakazi wa Gaza katika eneo hilo, pamoja na kuongezeka upinzani wa kimataifa dhidi ya mashambulizi na mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel ikisaidiwa na washirika wake wa Kimagharibi.

Suala jingine lililozungumzwa na Borrell ni ukosoaji wa nchi za Kusini kuhusu misimamo ya kinafiki na kindumakuwili ya nchi za Magharibi kuhusiana na vita vya Ukraine na vita vya Gaza. Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesisitiza kuwa nchi nyingi za Kusini zinashutumu nchi za Magharibi kwa kuendeleza sera za kindumakuwili katika masuala muhimu ya kimataifa.

Wamagharibi wananyamazia kimya mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel Ukanda wa Gaza

Ukweli ni kwamba, tofauti na msimamo wao mkali kuhusiana na vita vya Ukraine, nchi za Magharibi zimefumbia macho bali zimeunga mkono na kufadhili mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza. Nchi hizo za Magharibi, hususan Marekani, zimekuwa zikieleza mara kwa mara upinzani wao dhidi ya uamuzi wa kutambuliwa maafisa wa utawala wa Kizayuni Israel hususan Netanyahu kuwa ni watenda jinai za kivita huko Gaza, na wakati huo huo zinamtambua Putin kuwa anatenda jinai na uhalifu wa kivita huko Ukraine. 

Tags