May 19, 2024 11:25 UTC
  • Hatua mpya ya Baraza la Wawakilishi la Marekani katika kuunga mkono utawala wa Kizayuni

Alhamisi Mei 16, Baraza la Wawakilishi la Marekani, Congress, lilikosoa uamuzi wa hivi karibuni wa Rais Joe Biden wa Marekani wa kuzuia kutumwa shehena ya silaha kwa Israel, na kupasisha mswada chini ya anwani "Misaada kwa ajili ya Usalama wa Israel", ambao ulimtaka Biden asizuie tena kutumwa silaha Israeli kwa kisingizio chochote kile.

Kupasishwa mswada huo katika Baraza la Wawakilishi, ambalo linadhibitiwa na Warepublican wengi, kumefanyika kwa lengo la kupunguza uwezo wa Rais wa Marekani katika kuzuia kutumwa silaha Israel. Mswada huo ulipitishwa Alhamisi kwa kura 224 za ndio na  187 za kupinga.

Kupasishwa mpango wa kulisaidia jeshi la Israel ni radiamali ya kukabiliana na tishio la hivi karibuni la Ikulu ya White House la kusitisha kupelekwa silaha Israel iwapo utawala huo utauvamia mji wa Rafah. Wiki iliyopita  serikali ya Biden ilisimamisha mpango wa kutumwa shehena iliyokuwa na mabomu 3,500 ya pauni 2,000 na pauni 500 kwenda Israel kutokana na  wasiwasi wa kutumika silaha hizo huko Rafah. Mike Johnson Spika wa Congress amekaribisha kupasishwa mpango huo, na wakati huohuo kukosoa uamuzi wa utawala wa Biden wa kuzuia shehena hiyo ya silaha kupelekwa Israel. Amesema: "Uamuzi wa serikali ya Biden wa kuzuia kutumwa silaha (Israel) ni msiba na jambo ambalo limefanyika  kinyume kabisa cha  matakwa ya Congress." Amesema kupitishwa mpango huo ni "ujumbe wa wazi wa mshikamano na uungaji mkono wa nchi hiyo kwa Israel" na kusisitiza kuwa Congress inataka kufikishwa haraka silaha hizo Israel kwa ajili ya kulinda mshirika wake muhimu  zaidi katika Mashariki ya Kati.

Silaha za Marekani zinazotumwa Israel

Kwa mujibu wa waledi wa  mambo, kupasishwa mpango wa kuiunga mkono kijeshi Israel katika Baraza la Wawakilishi la Marekani inahesabiwa kuwa hatua ya kupinga tu siasa za serikali ya Biden kuhusu vita vya Gaza, ambapo mpango huo bado unahitajia idhini ya Seneti ya Marekani, ambayo inadhibitiwa na Wademocrat. Kwa hivyo, kuna uwezekano mdogo wa kupasishwa kuwa sheria. Mswada huo unaonyesha kuwepo mgawanyiko mkubwa nchini Marekani kuhusu suala la kuendelea kutolewa uungaji mkono kwa Israel, na uwezekano wa kupita kwake kutazidisha tu hitilafu kati ya vyama viwili hivyo katika mwaka huu wa uchaguzi wa rais nchini humo.

Hata hivyo, siasa za serikali ya Biden katika kusimamisha baadhi ya misaada ya silaha kwa Israeli, ikiwa ni pamoja na mabomu ya kulenga shabaha na kuvunja miamba, zimechukuliwa katika fremu ya mzozo kati ya Washington na Tel Aviv kuhusu kuendelea vita vya Gaza, hasa uamuzi wa jeshi la Israel wa kushambulia mji wa Rafah kusini mwa Gaza jambo ambalo limewakasirisha Warepublican. Baadhi ya wawakilishi wa Republican wanasema kuwa kwa uamuzi wake huo Rais Joe Biden ameupa kisogo utawala wa Israel.

Pamoja na hayo, madai ya Warepublican kuwa Biden haiungi mkono Israel vya kutosha yana sura ya kisiasa na ushindani wa vyama kuliko kitu kingine chochote, kwa sababu tokea kuanza vita vya Gaza, Marekani imekuwa ikiuunga mkono utawala wa Kizayuni waziwazi na kwa njia isiyo na mfano wake katika ngazi zake zote. Kuhusiana na hilo, Kanali ya 11 ya utawala wa Kizayuni iliripoti Alhamisi jioni kwamba shehena ya kwanza ya silaha za Marekani, ambayo serikali ya Biden ilidai kuwa imeizuia, tayari imewasili Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Hii ni katika hali ambayo wiki iliyopita, serikali ya Biden ilidai kusimamisha kutuma baadhi ya vifurushi vyake vya msaada wa silaha kwa utawala huo katika kupinga kile kilichodaiwa kuwa kupinga hatua ya jeshi la Israel ya kuanzisha operesheni huko Rafah.

Tags