Aug 09, 2024 12:01 UTC
  • Ombi la Guterres la kutokomezwa silaha za nyuklia, siku ya kumbukumbu ya mauaji ya Hiroshima

Katika kuadhimisha mwaka wa 79 wa shambulio la bomu la atomiki lililofanywa na Marekani huko Hiroshima, Japan, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ametoa wito wa kutokomezwa silaha za nyuklia duniani kote na kuahidi kwamba Umoja wa Mataifa hautaacha juhudi za kuhakikisha kwamba maafa ya siku hiyo hayarudiwi tena.

Guterres amesisitiza kuwa, tishio la kutumia silaha za nyuklia halishuhudiwi tu katika vitabu vya historia, bali ni hatari halisi na ya sasa, ambayo inaonekana tena katika matamshi ya kila siku kwenye uhusiano wa kimataifa.

Antonio Guterres

Onyo hilo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hatari ya kutumia silaha za nyuklia ni ukweli mchungu ambao ulimwengu uliwahi kuuonja huko Japan. Mashambulio ya mabomu ya nyuklia yaliyofanywa na Marekani huko Hiroshima na Nagasaki nchini Japan wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, ilikuwa jinai mbaya dhidi ya ubinadamu, ambayo iliua na kujeruhi mamilioni ya watu, na hadi sasa watu wa Japan bado wanakabiliana na athari zake mbaya kwa binadamu.

Ali Rohafza, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, anasema kuhusu suala hili kwamba: "Shambulio la mabomu ya nyuklia la Marekani dhidi ya Japan lilionyesha kwamba ubinadamu hauna usalama unaohitajika na kwamba wahalifu wanaweza kutumia mabomu ya atomiki wakati wowote kwa malengo yao maovu. Kwa sababu hiyo, wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kutokomezwa silaha za nyuklia duniani unapaswa kutambuliwa kuwa mpya, na kumbukumbu ya mauaji ya Hiroshima haipaswi kutazamwa kama tukio la kimaonyesho."

Onyo la Guterres linatia wasiwasi kwa sababu, kwa mujibu wa matamshi yake, ibra na funzo la shambulizi la Hiroshima, ambalo linahimiza amani na kutokomezwa silaha za nyuklia, limewekwa kando, na baadhi ya duru za kisiasa na kijeshi bado zinazungumzia uwezekano wa kutumia mabomu ya atomiki. Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, matumizi ya silaha za nyuklia hayakubaliki, na vita vya nyuklia havina mshindi.

Hiroshima baada ya kushambuliwa kwa bomu la nyuklia la Marekani

Wakati huo huo, katika upande mmoja madola makubwa yanatekeleza sera za kibaguzi kuhusiana na teknolojia ya nyuklia kwa kuzuia baadhi ya nchi kupata maarifa ya matumizi ya amani ya teknolojia hiyo; na kwa upande mwingine, zinahatarisha usalama wa dunia kwa kuruhusu baadhi ya nchi kuwa na silaha za nyuklia, ukiwemo utawala bandia wa Israel. 

Shughuli ya kumbukumbu ya mauaji ya Marekani huko Hiroshima hufanyika kila mwaka nchini Japan; hata hivyo, inaonekana kwamba jamii ya kimataifa haijajifunza kutokana na matokeo mabaya ya shambulio la atomiki huko Japan kwa ajili ya kuimarisha utulivu na amani duniani, na hali ya kutoaminiana na migawanyiko inaongezeka duniani kote, na mfano wa tishio la usalama wa kimataifa unaweza kuonekana katika kipindi cha sasa, hasa kutoka kwa utawala wa kibaguzi na kigaidi wa Israel.

Kwa vyovyote vile, watu wa Japan ndio wahanga wa kwanza wa bomu la atomiki, na Marekani ambayo ilifanya uhalifu mkubwa zaidi dhidi ya ubinadamu kwa kudondosha mabomu ya atomiki huko Hiroshima na Nagasaki, bila aibu, inaendelea kuunda silaha mpya za nyuklia. Hii ina maana kwamba, Marekani haijutii kuua mamilioni ya watu wa Japan, lakini pia inaendelea kutishia usalama wa kimataifa kwa kuimarisha maghala yake ya silaha za nyuklia. Mwenendo huu wa Marekani umeyahamasisha mataifa mengine yenye nguvu za nyuklia kujaribu kusasisha silaha zao za atomiki. Ni kwa sababu hii, ndiyo maana wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kuangamizwa silaha za nyuklia kote duniani unapata maana na umuhimu mkubwa zaidi.