Aug 11, 2024 13:40 UTC
  • Takwa la Waislamu wa Marekani kwa Biden la kulaani ugaidi wa kiserikali wa Israel

Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR) limemtaka Rais Joe Biden wa nchi hiyo ajibu na kulaani vitendo vya ugaidi wa kiserikali vinavyofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Baraza hilo la Waislamu wa Marekani limesema: Iwapo Rais Biden anajali chochote juu ya uhai wa mwanadamu, anapaswa kutoa jibu dhidi ya kitendo hiki cha ugaidi wa kiserikali na kuacha kuupelekea silaha utawala wa Kizayuni, na pia kumlazimisha (Benjamin) Netanyahu akubali makubaliano ya usitishaji vita ambayo amekuwa akiyakanyaga.

Kadhalika kundi hilo la kutetea haki za Waislamu na kiraia nchini Marekani limeeleza kusikitishwa na hali mbaya ya watoto katika Ukanda wa Gaza, na kusisitiza kuwa, jamii ya kimataifa ina wajibu wa kusimamisha mauaji ya watoto katika eneo hilo la Palestina lililozingirwa. Katika shambulio la kinyama la Israel dhidi ya kambi ya wakimbiizi ya al Daraj katika Ukanda wa Gaza takribani Wapalestina 200 waliuawa shahidi.

Ofisi ya habari ya serikali ya Palestina huko Gaza imeilaumu Marekani na utawala wa Kizayuni kwa jinai hiyo ya kutisha. Hamas sambamba na kuashiria njama za Israel za kutaka kuhalalisha jinai hiyo ya kutisha ambayo imekabiliwa na wimbi la ukosoaji wa jamii ya kimataifa imetangaza kuwa, tunasisitiza kwamba hakukuwa na mtu hata mmoja aliyekuwa na silaha miongoni mwa mashahidi wa jinai ya shule ya Tabi'in na watu wote walikwenda katika shule hiyo kwa ajili tu ya kutekeleza ibada ya Sala ya Alfajiri.

 

Nukta inayotoa mguso ni radiamali ya serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani kwa uhalifu huu wa kutisha na ambao haujawahi kutokea. Katika radiamali yake kwa jinai mpya iliyofanywa na Wazayuni maghasibu dhidi ya watu madhulumu wa Gaza, Ikulu ya White House imedai: "Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu ripoti kwamba raia wameuawa huko Gaza kufuatia shambulio la wanajeshi wa Israel kwenye kambi moja iliyojumuisha shule piai!"

Pasi na kuashiria utumaji silaha usio na kikomo wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni kwa ajili ya kuwaua watu wa Palestina, Ikulu ya White imetangaza kuwa, tunawasiliana na wenzetu wa Israel ambao walisema kwamba maafisa wakuu wa Hamas walilengwa, na tumo katika kuomba maelezo zaidi ya tukio hili." Ikulu ya White House imekiri kwamba, raia wengi wanaendelea kuuawa na kujeruhiwa katika vita vya Gaza.

Kamala Harris, Makamu wa Rais wa Marekani na mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democratic katika uchaguzi ujao baadayr mwaka huu, ametosheka tu na kuelezea kwa maneno wasiwasi wake juu ya kulengwa kwa raia katika uhalifu wa hivi karibuni katika shule ya "Tabi'in" na amekataa kuunga mkono takwa la kusitishwa kupelekewa silaha Israel.

Licha ya wasiwasi ulioonyeshwa na utawala wa Biden, lakini kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Marekani ni kuwa, bomu lililotumiwa katika shambulio hilo lilitengenezwa Marekani.

Kanali ya Televisheni ya CNN iliripoti kuwa, bomu la kuongozwa la Marekani la GBU-39 lilitumiwa katika shambulizi la bomu katika shule ya Tabi'i huko Gaza na jeshi la utawala wa Kizayuni, ambalo lilisababisha kuuawa shahidi kwa takriban watu 200 na makumi ya wengine kujeruhiwa. Kwa muktadha huo, Marekanin ni mshirika wa moja kwa moja wa utawala wa Kizayuni katika mauaji ya watu madhulumu wa Gaza.

Rais Joe Biden wa Marekani

 

Ukweli wa mambo ni kuwa, Marekani imekuwa na sera za kindumakuwili na za nyuso mbili katika kuamiliana na Israel. Katika hali ambayo, idadi kubwa ya wabunge wa Kongresi wanapinga kuuziwa silaha utawala wa Kizayuni, Ikulu ya White House inaendelea kutilia mkazo suala la kuzatitiwa kwa silaha Tel Aviv na inatuma shehena kubwa za zana za kivita zenye nguvu kwa utawala wa Kizayuni ili kuwaua wananchi wanaodhulumiwa wa Gaza.

Hapana shaka kuwa, uungaji mkono wa pande zote wa Ikulu ya White House kwa Tel Aviv daima umekuwa taa ya kijani kwa utawala wa Kizayuni ya kuendelea na vitendo vyake vya jinai hususan mauaji ya kimbari ya watu wa Gaza na kutumia njaa katika Ukanda wa Gaza kama silaha ya kuwaulia Wapalestina wa Ukanda huo.

Lililo dhahir shahiri ni kuwa, madola ya Magharibi hususan Marekani na ya Ulaya ambayo kila mara yanafuata misimamo ya undumakuwili katika masuala ya ugaidi, haki za binadamu, jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu, mara hii pia hayajaonyesha radiamali ya maana ya mauaji dhidi ya Wapalestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni, bali yanmetosheka tu na kueleza wasiwasi au kulaani kwa maneno matupu jinai hiyo huku yakiendelea kuiunga mkono Israel katika nyanja zote.

Tags