Takwa la Pakistan la kutofanya biashara ya mafuta na utawala wa Kizayuni
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Pakistan amelaani kuuawa shahidi Ismail Haniye aliyekuwa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na kuelezea wasiwasi wake mkubwa alionao kuhusiana na chokochoko zinazoongezeka za utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Asia Magharibi.
Akihutubia hivi karibuni katika kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Ishaq Dar sambamba na kutangaza uungaji mkono wake kwa misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa wito wa kususia kufanya biashara na utawala huo ghasibu katika sekta ya mafuta. Amezitaka nchi wanachama wa OIIC kutofanya biashara ya mafuta na utawala wa Israel unaotenda jinai kila uchao dhidi ya wananchi wa Palestina. Naibu Waziri Mkuu huyo wa Pakistan ametilia mkazo mshikamano imara baina ya Tehran na Islamabad.
Pakistan daima imekuwa pamoja na wananchi wa Palestina na imetangaza dhamira yake ya kuunga mkono malengo ya Wapalestina ya kupigania ukombozi wa ardhi zao kutoka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel unaozikalia kwa mabavu ardhi zao. Kwa muktadha huo, tangazo la uungaji mkono wa afisa mkuu wa Pakistan kwa Palestina na misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuelekea hilo ni msimamo halisi.
Mehdi Jamali, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Ikitokea kuwa na mshikamano wa kweli baina ya nchi za Kiislamu dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Kizayuni, bila shaka ulimwengu wa Kiislamu utaibuka na ushindi dhidi ya utawala huo ghasibu na waungaji mkono wake."
Iwapo nchi nyingine za Kiislamu zitachukua msimamo unaofanana na ule wa Pakistan kuhusiana na jinai za utawala wa Kizayuni, utawala huu hautathubutu kuwaua watu wanaodhulumiwa wa Gaza. Ni kutokana na sababu hiyo, ndio maana kwa mtazamo wa Pakistan ni kuwa, ni haki ya Iran na Palestina kulipiza kisasi dhidi ya utawala unaoukalia kwa mabavu wa Israel kwa jinai dhidi ya ubinadamu, na wakati huo huo ni lazima tuwe makini na mipango ya kivita ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu mtenda jinai wa utawala huo wa Kizayuni.
Kwa sababu viongozi wenye msimamo mkali wa Israel wanatafuta kupanua vita katika eneo hilo kwa ajili ya kuendeleza maisha yao ya kisiasa. Lakini kinachoupa nguvu utawala unaoukalia kwa mabavu wa Quds ni uungaji mkono wa pande zote wa Marekani, ambao umemfanya Netanyahu kuchukua hatua za kuwaua bila hatia yoyote raia wa Palestina.
Kwa mujibu wa Mohammad Is'haq Dar, mauaji ya kiongozi wa harakati ya Hamas mjini Tehran aliyekuja kushiriki hafla ya kuapishwa Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Masoud Pezeshkian ni kitendo kibaya na cha kinyama dhidi ya amani na utulivu wa eneo hili na vyovyote tukakavyolaani jinai hii bado itakuwa haitoshi.
Kwa hiyo, wakati umefika wa kuwawajibisha Wazayuni, na ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kuchukua hatua ambayo ni zaidi ya kutoa kauli za kulaani na kukemea jinai za Israel. Kwa muktadha huo, kama utawala wa Kizayuni wa Israel hautakubali makubaliano ya kusitisha mapigano mara moja huko Gaza, wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu lazima wachukue hatua ya kuuwekea vikwazo na na kutofanya nao biashara ya mafuta.
La kusikitisha zaidi ni kwamba, baadhi ya nchi za Kiislamu zinalaani kwa maneno tu jinai za utawala wa Kizayuni, lakini kivitendo zinaendeleza uhusiano wao wa kibiashara na utawala huo iwe ni wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja, huku nchi za Kiislamu zikiwa na nyenzo ambazo zinaweza kuzitumia kuushinikiza utawala wa Kizayuni kusitisha mara moja vita huko Gaza, ambayo ni mafuta na bidhaa nyingine zinazotokana na nishati hiyo.
Hapana shaka kuwa kuendelea jinai za utawala ghasibu wa Israel huko Gaza ni sawa na kufanya mauaji ya kimbari. Sambamba na mauaji hayo, Israel inatumia njaa kama silaha dhidi ya Wapalestina. Kwa hivyo, haikubaliki kwa Waislamu kwamba nchi za Kiislamu zitoe tu maazimio na taarifa za kulaani jinai za utawala wa Kizayuni na kutotumia nguvu na zana zao dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.