Sep 09, 2024 06:49 UTC
  • Erdogan atoa mwito wa kuanzishwa 'Muungano wa Kiislamu' wa kukabiliana na Israel

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ametoa wito wa kuundwa muungano mpana wa nchi za Kiislamu ili kukabiliana na alichokiita "tishio la kujitanua" linaloonekana kutoka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Erdogan ametoa mwito huo alipohutubia hafla ya Jumuiya ya Skuli za Kiislamu iliyofanyika nje ya mji wa Istanbul.
 
Rais wa Uturuki amesema: "hatua pekee ambayo itazuia kiburi cha Israel, ujambazi wa Israel, na ugaidi wa serikali ya Israel ni muungano wa nchi za Kiislamu," na akaongezea kwa kusema, Ankara tayari imechukua hatua hivi karibuni zenye lengo la "kuanzisha mstari wa mshikamano dhidi ya tishio linaloongezeka la upanuzi" kwa kutaka kurekebisha uhusiano wake na Syria na Misri.
Rais Erdogan wa Uturuki (kulia) akiamkiana na Rais El Sisi wa Misri

Erdogan ameushutumu utawala ghasibu wa Israel kwa kutaka vitokee vita vikubwa vya Mashariki ya Kati ili uyateke na kuyakalia kimabavu maeneo zaidi ya eneo hilo. Ameipongeza harakati ya Muqawama ya Palestina Hamas, akisema imekuwa ikipigana na Israel "kwa niaba ya Waislamu" na "kutetea ardhi za Kiislamu," ikiwa ni pamoja na Uturuki.

Aidha, Rais wa Uturuki ametoa indhari na kutanabahisha kwamba, Israel haitakomea Ghaza na akasema: "iwapo Israel itaendelea kwa namna hii, itaweka malengo yake kwingine baada ya kuikalia kwa mabavu Ramallah. Zamu itakuja kwa nchi zingine katika kanda. Itakuja kwa Lebanon na Syria. Na wataelekeza macho yao kwenye nchi yetu ya asili iliyopo kati ya Tigris na Euphrates”.../