Serikali ya Australia kupitisha sheria ya kupiga marufuku vijana wadogo kutumia mitandao ya kijamii
(last modified 2024-09-11T02:20:39+00:00 )
Sep 11, 2024 02:20 UTC
  • Serikali ya Australia kupitisha sheria ya kupiga marufuku vijana wadogo kutumia mitandao ya kijamii

Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese ametangaza kuwa serikali yake inapanga kupiga marufuku watoto kutumia mitandao ya kijamii.

Katika taarifa aliyotoa jana Jumanne Albanese alisema, serikali yake ya chama cha Leba itapitisha sheria mwaka huu kuweka mpaka wa umri wa chini unaoruhusiwa kutumia mitandao ya kijamii na majukwaa mengine muhimu ya kidijitali.
 
Katika taarifa yake hiyo, waziri mkuu wa Australia amesema: "tunajua kwamba mitandao ya kijamii inasababisha madhara ya kijamii, na inawaweka mbali watoto na marafiki wa kweli na tajiriba za maana".
 
Hata hivyo, Albanese hakutoa maelezo zaidi kuhusu kikomo cha umri kwa watoto ambao hawataruhusiwa kutumia mitandao ya kijamii.

Aidha amebainisha kuwa, mbinu inayoongozwa na Jumuiya ya Madola katika suala hilo muhimu la kijamii itahakikisha watoto wa Australia wanalindwa vyema dhidi ya madhara ya mitandao ya kijamii, na wazazi na walezi wa watoto wanasaidiwa.

 
Siku ya Jumapili, vyombo vya habari vya Australia viliripoti kwamba Australia Kusini imetayarisha sheria mpya ambayo itawalazimisha wamiliki wa mitandao ya kijamii kuwapiga marufuku watoto walio na umri wa chini ya miaka 14 kutoka kwenye majukwaa yao au mitandao hiyo kukabiliwa na adhabu.
 
Kwa mujibu wa ABC News, sheria hiyo mpya inaweza kufuatwa katika majimbo mengine ya Australia.
 
Waziri Mkuu wa Australia Kusini Peter Malinauskas amesikika akisema, "serikali sasa itaingilia kati, tutapiga marufuku watoto kupata njia za kuzifikia akaunti hizi".../

 

Tags