Safari ya pamoja ya mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Uingereza nchini Ukraine
Anthony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amefanya safari ya pamoja na mwenzake wa Uingereza David Lemmy nchini Ukraine kwa ajili ya kuongeza misaada ya kijeshi na kifedha ya nchi za Magharibi kwa nchi hiyo katika vita vyake dhidi ya Russia.
Wametangaza rasmi kwamba lengo la safari yao ni kusisitiza kuendelea uungaji mkono wa Washington na London kwa Kyiv dhidi ya Russia na kuhakikisha kwamba maendeleo ya kijeshi, kiuchumi na kidemokrasia yanapatikana kwa manufaa ya Ukraine. Safari ya mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Uingereza nchini Ukraine imekuja wakati nchi hiyo si tu imeshindwa kupata mafanikio yoyote yaliyotarajiwa na nchi za Magharibi katika vita na Russia, bali imezikatisha tamaa nchi za Ulaya kutokana na matokeo hasi ya vita licha ya kupewa misaada mingi ya kifedha na kijeshi na nchi za Magharibi.
Kwa hiyo kwa kufanya safari ya pamoja, Blinken na Lemy wanajaribu kuzitia moyo na kuzihimiza nchi hizo ziendelee kuipa Ukraine misaada ya kifedha na kijeshi bila kusita.
Moja ya masuala ya kijeshi yaliyoibuliwa karibuni na Ukraine ni kwamba nchi za Magharibi ziiruhusu kutumia makombora ya masafa marefu kulenga maeneo ya Russia. Moscow imesema suala hilo linaweza kueneza vita vya Ukraine hadi Ulaya.
Ingawa hadi sasa Russia imeonyesha subira kubwa na kujizuia kuchukua hatua yoyote muhimu katika kukabiliana na utumaji wa silaha za Magharibi nchini Ukraine, lakini itakuwa vigumu kwa nchi hiyo kuendelea kuonyesha subira hiyo iwapo Marekani na nchi za Magharibi zitairuhusu Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu kulenga maeneo yake.
Moscow inachukulia shambulio lolote la Ukraine katika maeneo ya ndani kabisa ya ardhi ya Russia kuwa ishara ya kuingia moja kwa moja na kwa pamoja nchi za Magharibi katika vita hivyo, jambo ambalo bila shaka litakuwa na matokeo hatari na yasiyotabirika.