Sep 15, 2024 03:49 UTC
  • Mwanadiplomasia wa Marekani aonya kuhusu nia ya Israel ya kuzikalia kwa mabavu nchi za Kiarabu

Balozi wa zamani wa Marekani nchini Saudi Arabia ametahadharisha kuhusu dhamira ya kupenda kujitanua ya Israel na kusema kuwa, itikadi za kidini za Mayahudi wenye misimamo mikali zinaitaka Israel kujitanua nje ya Palestina ili kutawala nchi nyingine za Mashariki ya Kati.

Chas W. Freeman Jr. amesema kwamba, Israel inataka kudhibiti eneo kubwa la Mashariki ya Kati hatua kwa hatua. Ameongeza kuwa: "Mwishowe, Israel ina lengo sio tu kuwafukuza Wapalestina katika nchi yao, lakini pia kutawala eneo zima la Asia Magharibi."

Balozi wa zamani wa Marekani nchini Saudia amesisitiza kuwa, kuna beji ya kijeshi inayovaliwa na baadhi ya watu katika Jeshi la Ulinzi la Israel "inayoonyesha Israel Kubwa, ambayo inajumuisha sehemu za Misri, kaskazini mwa Saudi Arabia, Jordan yote, Syria, Lebanon, na hata sehemu ya Iraq inayojumuisha Mto Furati (Euphrates)."

Mwanadiplomasia huyo wa Marekani ameeleza kwamba, kwa Wazayuni wenye itikadi za kidini, ardhi hiyo iliahidiwa kwa Wayahudi na Mungu.

Katika muktadha huo, hivi karibuni televisheni ya al Jazeera ya Qatar ilimnukuu Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan akisema, "Israel itatugeukia baada ya kukalia kwa mabavu Ramallah, na ikiwa itaendelea kwa njia hii, itaelekeza mazingatio yake mahali pengine, mpaka Lebanon, Syria, na ardhi yetu ya kati ya Mto Furati na Nile.”